NAOT

CAG ahudhuria kikao cha 67 cha Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa (UNBOA)

 

 


http://t0.gstatic.com/images?q=tbn:ANd9GcTx3DFP4tmfv__5sdQRQ9SWB8y_hWZUrgNOl_y6c0FUM6YdmHc&t=1&usg=__0cK8dRlxilrVQLCE9o136zMfVjI=

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA TAIFA YA UKAGUZI

NAO LOGO_1

 

 

Taarifa kwa Vyombo Vya Habari

 

CAG AHUDHURIA KIKAO CHA 67 CHA BODI YA UKAGUZI YA

UMOJA WA MATAIFA (UNBoA)

 

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Ludovick S. L. Utouh ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa (UNBoA), kwa siku mbili (2) amehudhuria kikao cha 67 cha Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa kilichofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kuanzia tarehe 23 hadi 24 Julai, 2013 mjini New York, Marekani.

 

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe wote watatu (3) ambao ni China, Tanzania na Uingereza wanaounda Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa, ripoti kumi na tano (15) za Ukaguzi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2012 zilisainiwa na wajumbe hao chini ya uenyekiti wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Uingereza.

 

Tanzania inayowakilishwa na CAG, Bw. Ludovick S. L. Utouh ilikuwa ni mara yake ya kwanza kukagua Hesabu za Umoja wa Mataifa (UN) ambapo kati ya ripoti kumi na tano (15) zilizosainiwa ripoti sita (6) za ukaguzi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa zilifanywa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ya Tanzania (NAOT) na kukubalika na Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa.

 

Mashirika sita (6) ya Umoja wa Mataifa yaliyokaguliwa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ya Tanzania ni pamoja na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Idadi ya Watu Duniani la Umoja wa Mataifa (UNFPA), Shirika la Ujenzi na Misaada la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi wa Palestina na Mashariki (UNRWA), Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa UNRWA Wakazi (UNRWA – SPF), Shirika la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN – Women) na Shirika la Ukuzaji Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF).

 

Ripoti tisa (9) za Ukaguzi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa zilizosalia zilitokana na ukaguzi uliofanywa na Ofisi za Ukaguzi za Hesabu za Serikali za China na Uingereza.

 

Ripoti hizo ni za Ukaguzi wa Ujenzi wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (CMP), Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Usaidizi wa Miradi (UNOPS), Mfumo wa Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (Umoja 2012), Taarifa ya Maendeleo ya Utekelezaji wa Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Hesabu kwa Taasisi za Umma (IPSAS) katika Umoja wa Mataifa, Taarifa ya Utekelezaji wa Mapendekezo ya Ukaguzi kwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Escrow Akaunti ya Umoja wa Mataifa, Mfuko wa Pamoja wa Akiba ya Uzeeni wa Watumishi wa Umoja wa Mataifa.

 

Katika ziara yake Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na ujumbe wake , Ijumaa , Julai 26, 2013 ulifanya mazungumzo na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Mhe. Balozi Tuvako Manongi, kwenye Ubalozi wa Tanzania uliopo mjini New York, Marekani.

 

CAG alimjulisha Mhe. Balozi Manongi madhumuni ya ziara yake na umuhimu wa fursa ya Ukaguzi wa Umoja wa Mataifa kwa Tanzania ikiwa ni pamoja na:-

(i)          Kuitangaza nNchi yetu ya Tanzania ulimwenguni kote kunakofanyika ukaguzi huu.

(ii)        Kujenga uwezo na uelewa wa Wakaguzi zaidi ya nia moja kwa wakati wanaohusika na ukaguzi huu wa kimataifa.

(iii)       Kuwakomboa kiuchumi Wakaguzi wanao shiriki kwenye ukaguzi wa UN

(iv)       Kuiongezea Ofisi fursa ya kupata kazi nyingine za ukaguzi wa Mashirika/Taasisi za kimataifa.

(v)         Kuongeza ufanisi na ubora wa ukaguzi wa Serikali na taasisi zake hapa nyumbani.

Ukaguzi katika Mashirika Mengine ya Kimataifa.  Kwa muda mrefu Ofisi imekuwa inashiriki pamoja na Ofisi za Ukaguzi za nchi za SADC kuikagua SADC ambayo makao yake makuu yako Gaborone Botswana.

 

Vile vile tangu kuanzishwa upya kwa Jumuiya  ya Afrika Mashariki, Ofisi kwa kushirikiana na Wakaguzi Wakuu wa Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi tumekuwa tunaikagua Jumuiya hiyo kila mwaka.

 

Ofisi kutokana na uzoefu iliokwisha kupata katika ukaguzi wa taasisi hizi za kimataifa, itaendelea na juhudi za kutafuta kazi nyingine katika taasisi hizo ili kuendelea kuimarisha utendaji wa Wakaguzi wake.

 

KITABU CHA MUHTASARI WA RIPOTI  ZA CAG ZA MWAKA 2011/2012

 

Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imetoa kitabu cha Muhtasari wa Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu kwa mwaka 2011/2012 kwa mara ya kwanza.

 

Wananchi na jamii kwa ujumla wanayo haki ya kikatiba kupata taarifa sahihi za Serikali kuhusu utekelezaji wa sera, mipango na miradi mbali mbali ya maendeleo  kupitia vyombo vya habari na njia nyingine za mawasiliano.

 

Ingawa  ripoti ninazozitoa kila mwaka zipo kwa lugha za kiingereza na kiswahili, bado ripoti  hizi zinakuwa ni kubwa na kuzifanya zisiwe rahisi kusomeka.  Vile vile  kumekuwepo na upotoshaji wa taarifa hizi kwa namna zinavyotumiwa na wadau mbali mbali.  Katika  kutafuta suluhisho la tatizo hili, Ofisi ya Taifa ya  Ukaguzi  kwa mara ya kwanza imeandaa muhtasari wa ripoti zote za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zilizowasilishwa Bungeni tarehe 11 Aprili, 2013.  Madhumuni ya kuandaa kitabu hiki ni:

(i)                Kurahisisha usomaji na uelewa wa Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi      Mkuu waHesabu za Serikali.

 

(ii)             Kurahisisha  upatikanaji wa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu   wa Hesabu za Serikali.

 

Ofisi itaendelea kuboresha  mawasiliano  na wadau wake wote, ili Watanzania walio wengi waweze kupata taarifa hizi, kuzisoma na kuzielewa.  Ofisi itashukuru kupata mawazo yeyote ya kuboresha zaidi mawasiliano yetu na wadau wetu.

 

PONGEZI KWA SPIKA

 Napenda kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Anne  Makinda (Mb) na Spika wa Bunge la Tanzania kwa uamuzi wake wa kupanga upya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) ambapo sasa kuna PAC I na PAC II ambapo PAC I  itashughulikia taarifa za hesabu  za Serikali Kuu, Idara zinazojitegemea na Taasisi nyingine za Serikali (MDAs) wakati PAC II itashughulikia taarifa za hesabu za Mashirika ya Umma (Parastatals).  Katika mpangilio huo, PAC I itakuwa chini ya uenyekiti wa Mh. Zitto Kabwe (Mb) wakati PAC II itakuwa chini ya uenyekiti wa Mh. Deo Filikunjombe (Mb).

 

Tunaamini kuwa utaratibu huu utaleta ufanizi na tija katika utendaji  kazi wa Kamati ya PAC na hivyo kuchangia  kwa kiasi kikubwa uimarishaji wa uwazi na uwajibikaji katika kusimamia makusanyo na mapato ya fedha za umma.

 

USAHIHISHAJI WA RIPOTI ZA VYOMBO VYA HABARI KUHSU HALI YA HESABU ZA WIZARA YA UJENZI ZA MWAKA 2011/2012 (FUNGU 98)

 

Baada ya taarifa ya ukaguzi kuwasilishwa Bungeni kwa mujibu wa Ibara ya 143 (4)   ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na pia kwa mujibu  wa  kifungu Na.39  cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na.11 ya mwaka 2008, taarifa hizi zilianza kufanyiwa kazi  na Kamati za kudumu za Bunge za PAC na LAAC kuanzia juma lililopita.

 

Kamati ilipokuwa ikiliendelea kuzifanyia kazi ripoti hizi, juma lililopita kumekuwepo na upotoshaji wa taarifa kuhusu  taarifa za hesabu a Wizara ya Ujenzi (Fungu 98).  Kulikuwepo kwenye vyombo vya habari mbali mbali taarifa zisizo sahihi kuwa  kulikuwepo na ufisadi katika matumizi  ya fedha za umma kewnye Wizara hiyo.  Usahihi wa taarifa hizo ni  huu hapa chini:

 

·        Kiasi cha Sh.252,975,000 kilichohojiwa na ukaguzi ni fedha ambazo zimeonyeshwa kwenye taarifa za hesabu za Wizara  kama vile ni miradi mipya ya mwaka 2011/2012 tofauti ni uhalisia wenyewe ulivyo. Uhalisia ulivyo ni kwamba fedha hizi baada ya kupokelewa na Wizara ya Ujenzi  kutoka Hazina zilihamishwa kwenda Wakala wa Barabara (TANROADS) kulipia madeni ya Makandarasi wa miradi ya barabara zilizotekelezwa na wakala wa barabara ambao walikuwa hawajalipwa kwenye mwaka wa fedha wa  2010/2011. 

·        Fedha hizi Sh.252,975,000 kimakosa zilijumuishwa kwenye hesabu za Wizara kama matumizi ya akaunti ya maendeleo hivyo kuongeza matumizi ya Wizara kimakosa kwa kiasi hicho.  Kihasibu, fedha hizi Sh.252,975,000 zilipaswa kuonyeshwa kwenye hesabu za mtumiaji halisi wa fedha hizi ambaye ni Wakala wa Barabara (TANROADS)  na siyo Wizara.  Hivyo kwa sababu za Wizara hazikuwa sahihi na kwa kuwa ongezeko hilo la matumizi la Sh.252,975,000 lilikuwa kubwa (material) Wizara ilipewa hati ya ukaguzi yenye mashaka (Qualified Opinion)

 

Hivyo katika kujadili hesabu za Wizara ya Ujenzi hakukuwepo na tuhuma zozote za ufisadi ila Kamati ilimtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuihakikishia matumizi ya fedha hizo jambo ambalo litafanyika.

 

Mbali na dosari hiyo ya kihasibu Wizara ya Ujenzi inafanya kazi nzuri sana ya kusimamia na kujenga barabara katika kona zote za Nchi yetu.

Tuwapongeze kwa kazi nzuri wanayoifanya ili wawe na moyo wa kuchapa kazi zaidi kwa maendeleo ya nchi yetu.

 

Ninawashukuru kwa kunisikiliza na tafadhali nawaomba muwe makini zaidi katika matumizi ya maneno mazito kama ufisadi na namna mnavyoripoti mambo muhimu kwa wananchi.

 

Ahsanteni

 

 

 

PRESS RELEASE AUGUST 2013
PRESS RELEASE AUGUST 2013
PRESS RELEASE AUGUST 2013.doc
131.5 KiB
1112 Downloads
Details...
2013

Comments are closed.