NAOT

CAG AZINOA KAMATI YA PAC NA LAAC MOROGORO

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameshirikiana na wadau wa maendeleo kutoka Ujerumani (GIZ) na Canada CCAF kuandaa mafunzo kwa wajumbe wa kamati mpya za Bunge za Hesabu za Serikali ambazo ni Public Accounts Committee (PAC) na Local Authorities Accounts Committee (LAAC).

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Makamu Mwenyekiti wa Ukaguzi wa Ufanisi na Bunge wa Canada (CCAF) John Reed, amesema Kamati za Usimamizi za Bunge za Hesabu za Serikali, zinatakiwa kupewa mafunzo ya kutosha na muda mwingi wa kufanya kazi zake kwani zina wajumbe wapya ambao lazima wapate changamoto na ndiyo sababu wameshirikiana na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kuendesha warsha hii hapa nchini ili kuwasaidia viongozi hao kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa PAC Mhe. Aeshi Khalfan Hilaly (MB) alisema mafunzo haya ya siku tatu ni muhimu sana kwa kamati hizi ambazo ndio zinaanza rasmi kutekeleza jukumu lao la usimamizi kwa kutumia ripoti za CAG. Alieleza kuwa hivi karibuni wameshuhudia kupitia kwenye vyombo vya habari CAG amekabidhi ripoti yake ya Ukaguzi wa Mwaka 2014/15 ambapo itakabidhiwa bungeni na kuanza kutumiwa na kamati hizi kwa uchambuzi na usimamizi hivyo kuwepo mafunzo haya ni kipindi muafaka ili kuzipa ujuzi stahiki kamati hizi.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Assad (CAG) alisema ofisi yake imekuwa ikifanya mahusiano mazuri na CCAF ya Canada kwa ajili kuzijengea uwezo kamati hizo mbili nchini. “Tunatoa mafunzo kwa kamati hizi ili wawe na mbinu za kuhoji matumizi ya fedha za wananchi na kuwasilisha taarifa husika mahala husika,” alisema Prof. Assad.

Aidha CAG Prof. Assad aliongeza kuwa ni muhimu kwa Spika wa Bunge kuona ombwe ya usimamizi wa Mashirika ya Umma na hiyo kurejesha au kuunda kamati ya usimamizi nyingine ili kuwezesha shughuli zilizokuwa zikifanywa na kamati ya POAC zikaweza kuendelezwa. “Tunafahamu umuhimu wa kamati hiyo, leo tunaona umuhimu wa kazi zilizokuwa zikifanywa na kamati iliyovunjwa, hivyo Bunge linapaswa kuzingatia uamuzi unaofanywa,” alisema. Prof. Assad.

Pia, Prof. Assad aliwataka wabunge kuangalia upya Sheria ya Bajeti na kuunga mkono mapendekezo ya Ofisi yake ya kurekebisha kifungu cha 68 cha sheria hiyo kinachoinyima Ofisi ya CAG uhuru wa kifedha ambao pia unaathiri uhuru wa kiutendaji wa Ofisi yake. “Kifungu cha 68 cha Sheria Mpya ya Bajeti kinabadili uhuru wa CAG wa kifedha uliokuwa umetajwa kwenye Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya Mwaka 2008 hiyo kuathiri utendaji wa Ofisi ya CAG”, alifafanua Prof. Assad.

Naye Mwenyekiti wa LAAC, Mhe. Martin Msuha (MB) alisema kuwa ni matarajio yao mwisho wa warsha hii wataweza kuchambua ripoti za CAG kwa ufanisi zaidi pamoja na kuhoji Maafisa Masuuli ipasavyo. “Ili nidhamu irudi katika halmashauri zetu tuna haja ya kujengewa uwezo na kupewa muongozo wa masuala muhimu yaliyojitokeza kwenye kaguzi zenu ili tunapokutana na Maafisa Masuuli tuweze kuwawajibisha,” alisema.

Mafunzo hayo ni muhimu kwa ajili ya kuzijengea uwezo kamati hizo katika ukaguzi wa fedha za umma.

2016

Comments are closed.