NAOT

Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Watakiwa Kufanya Kazi kwa Bidii, Ueledi na Uadilifu

Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali imempokea Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bwana Charles Edward Kichere ambaye anachukua nafasi ya Profesa Mussa Juma Assad aliyemaliza muda wake.

Bwana Charles Kichere ambaye ameapishwa rasmi leo tarehe 4 Novemba, 2019, Ikulu Jijini Dar es salaam kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.

Uteuzi huo ulifanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na kisha kutangazwa na Katibu Mkuu  Kiongozi Balozi John Kijazi Ikulu Jijini Dar es salaam.

Aidha mara baada ya kuapishwa CAG alipata wasaa wa kuzungumza na baadhi ya viongozi na watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za jengo la Ukaguzi Dar Es Salaam

Akizungumza na watumishi hao, CAG alianza  kwa kuwashukuru kwa  mapokezi mazuri na pia aliwataka kila mmoja kuhakikisha anafanya kazi kwa bidii, ueledi, uadilifu na kuepukana na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za Serikali na kuachana na vishawishi vidogovidogo. CAG aliongeza kuwa hii itawezesha fedha kwenda kwenye mikondo sahihi ili zilete maendeleo kama vile ujenzi wa hospitali.

‘Wakaguzi waimarishe kaguzi zao hasa katika upande wa ukaguzi wa Serikali za Mitaa, usimamizi wa upande huo lazima uimarishwe. Rushwa na matumizi mabaya ya fedha za Serikali ni jambo kubwa, pia miradi ya maendeleo lazima isimamiwe na kufuatiliwa ili itekelezwe vyema’ amesema CAG.

Aidha alisema ‘leteni hoja zinazoisaidia Serikali na sio ziishie kwenu, niko tayari kufanya kazi na ninyi kwa ushirikiano, tuzungumze na kubadilishana mawazo, kila mmoja ana mchango wake katika kufanya kazi, kutekeleza na kutimiza wajibu wake kwa muda uliopangwa hasa katika kipindi hiki cha maandalizi ya ripoti kwa mwaka wa fedha ulioisha’.

Kwa Mujibu wa Ibara ya 143, (1-6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) (kama ilivyorekebishwa mara kwa mara) inaelezea kuhusu uteuzi na majukumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Wa Hesabu za Serikali (CAG) Bwana Charles Kichere (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi na watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi mara baada ya kuwasili katika Jengo la Ukaguzi Dar Es Salaam.

2019

Comments are closed.