NAOT

CAG na ukaguzi wa serikali kuu, serikali za mitaa na mashirika ya umma kwa mwaka 2015/16

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2016 imebaini kasoro na mapungufu mbalimbali katika ukaguzi wa serikali kuu, serikali za mitaa, mashirika ya umma na miradi ya maendeleo.

Akizungumza mara baada ya kuwasilishwa bungeni kwa ripoti hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Juma Assad ameeleza katika ripoti hizo zilizosomwa na mawaziri wa sekta mbalimbali amebaini mapungufu mbalimbali ikiwepo kutokuwepo kwa daftari la mali kwenye baadhi ya Ofisi za wakaguziliwa na hivyo kama mkaguzi kushindwa kuthibitisha ukamilifu wa taarifa za mali za kudumu.

“Katika ukaguzi wa vyama vya siasa nilioufanya ambao kimsingi ripoti yake inapatikana kwenye kitabu cha ripoti ya ukaguzi wa serikali kuu nimebaini kuwa Chama cha ACT Wazalendo hakikutunza vitabu vya fedha kama vile stakabadhi, daftari la fedha, daftari la leja, na daftari la mali za kudumu kwa ajili ya taarifa za fedha kinyume na Kifungu cha 14(10)(a) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, hali iliyomnyima uhuru mkaguzi na kupunguza mawanda ya ukaguzi”, alifafanua Prof. Assad.

Mapungufu mengine yaliyoonekana kwenye ukaguzi wa mwaka huu ni pamoja na Mfuko wa Rais wa Uwezeshaji ulipewa mkopo wa kiasi cha Sh. milioni 514 chini ya Mpango wa Taifa wa Uwezeshaji Kiuchumi ambazo pia hazikutumika kama ilivyokusudiwa.

Katika mapungufu mengine yaliyobainika ni pamoja na Wakala wa Majengo (TBA) kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma yenye thamani ya Tsh. milioni 178.718 kinyume na utaratibu huku wakala huo ukinunua vifaa vya ujenzi kutoka kwa watoa huduma bila kufuata utaratibu.

Kuhusu mwenendo wa hati za ukaguzi, Prof. Assad amesema katika mwaka wa fedha 2015/2016 ametoa jumla ya Hati 505, zinazohusu usahihi wa Hesabu zilizoandaliwa na mihimili mitatu ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama. Kati ya hizo, Hati zinazoridhisha ni 436 (86.34%); Hati zenye shaka ni 60 (11.88%); Hati zisizoridhisha ni nne (0.79%); na Hati Mbaya ni tano (0.99%).

Aidha, katika ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2015/2016 nimetoa hati za ukaguzi 797; ambapo Hati zinazoridhisha ni 725 (91%); Hati zenye shaka ni 71 (8.9%) na Hati mbaya ni moja (0.1%).

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameendelea kukutana na waandishi wa habari kila mwaka mara baada ya uwasilishaji wa ripoti zake. Ripoti za CAG ziliwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwishoni mwa mwezi Machi, 2017 kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusomwa bungeni tarehe 13 Aprili, 2017.

2017

Comments are closed.