NAOT

CAG – NI KOSA KUTUMIA RASIMU YA TAARIFA YA UKAGUZI WA MWAKA 2014/15

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa J. Assad imevionya vyombo vya habari kuacha kutumia rasimu ya ripoti yake ya mwaka 2014/15 kama ni taarifa rasmi kwani kufanya hivyo ni kupotosha umma wa Tanzania.

Akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari kwa niaba ya Prof. Assad, Naibu Mkaguzi Mkuu, idara ya Mashirika ya Umma Bw. Benjamin Mashauri hivi karibuni alisema ni kosa kutumia rasimu ya ripoti kuuhabarisha umma wa watanzania kwani taarifa zinazobebwa kwenye rasimu hiyo ni taarifa ambazo bado hazijakamilika.

“napenda kuvijulisha vyombo vya habari na Umma wa Watanzania kuwa Ukaguzi wa mwaka 2014/2015 kwa Serikali Kuu (Wizara, Idara, Balozi, Wakala), Mashirika ya Umma na Serikali za Mitaa haujakamilika. Ukaguzi wa taasisi hizi pindi utakapokamilika taratibu muhimu zitafanyika kulingana na matakwaya ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (iliyorekebishwa mara kwa mara ) ibara ya 143 pamoja na Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008”, alisema Mashauri.

Alifafanua kuwa, hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikinukuu baadhi ya rasimu ya taarifa ya CAG kimakosa kwani taarifa hiyo haina uhalali wowote na ni nukuu batili kwani taarifa ya CAG kwa ukaguzi wa mwaka 2014/15 bado haujakamilika. Alisistiza kuwa, chombo chochote kilichoripoti au kitakachoendelea kuripoti taarifa ya ukaguzi wa aidha wizara, idara na taasisi za serikali au shirika la umma kwa ukaguzi wa mwaka 2014/15 na kutumia rasimu ya ripoti ya CAG ya mwaka 2014/15 chombo hicho kitakuwa kinapotosha umma wa watanzania hivyo kukiuka sheria za nchi mna maadili ya kiutendaji ya taaluma yake. Alitaja baadhi ya taasisi zilizonukuliwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari ni rasimu ya ripoti yake ni pamoja Shirika la Maendeleo ya Mafuta na Gesi nchini (TPDC).

Kwa taarifa zaidi bofya link hii 2016 CAG – TPDC PRESS RELEASE Final FEBRUARY

2016

2 responses to “CAG – NI KOSA KUTUMIA RASIMU YA TAARIFA YA UKAGUZI WA MWAKA 2014/15”

 1. Godson Kapinga says:

  Tunashukuru kwa kutuelimisha maana kiukweli hata wengi tulivyoona ipo mitandaoni tumekuwa tukiipekua na kuisoma kama ndo taarifa rasmi. Hata hivyo napenda kufahamu zaidi ni wakati gani hutangazwa taarifa rasmi

  • Sarah says:

   Kwa mujibu wa Ibara ya 143 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CAG anapaswa kuwasilisha ripoti yake ya mwaka kwa Rais kabla ya mwezi Machi 31. Baada ya Rais kupokea taarifa hiyo, katiba inaelekeza kuwa itabidi iwasilishwe katika kikao cha bunge kabla ya kupita siku saba (7) tangu siku ile kilipoanza kikao hicho. Iwapo Rais hata chukua hatua za kuwasilisha taarifa hiyo kwenye Bunge, basi CAG atawasilisha taarifa hiyo kwa Spika wa Bunge (au Naibu Spika ikiwa kiti cha Spika ki wazi wakati huo au ikiwa kwa sababu yoyote Spika hawezi kutekeleza shughuli za kazi yake) ambaye atawasilisha taarifa hiyo kwenye bunge. Katika historia ya nchi yetu ya Tanzania hilo halijawahi kutokea.

   Kwa mwaka huu ripoti za CAG zimewasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 28 Machi 2016 na kusomwa bungeni 25 Aprili 2016 hivyo kuwa mali ya umma. Ripoti zote za CAG kwa lugha ya kiswahili nakiingereza zinapatikana kwenye tovuti yetu ya http://www.nao.go.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Captcha *