NAOT

DPP AELEZA WAJIBU WA WATAALAMU WA MASUALA YA SHERIA KATIKA TAASISI KUU ZA UKAGUZI AFRIKA

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, amewataka wataalam wa sheria katika Ofisi za Taifa za Ukaguzi barani Afrika washiriki kikamilifu katika kuhakikisha Ripoti za Ukaguzi zinaubora wa kutosha kutumika mahakamani kwa ushahidi pale zinapohitajika.

Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam leo alipokuwa akifungua warsha ya siku mbili kwa wanasheria wa Jumuiya ya Taasisi Kuu za Ukaguzi barani Afrika kwa nchi zinazozungumza lugha ya kiingereza (AFROSAI-E).

“Haya yote yanahitaji ujuzi wa kutosha ili kuwa wanasheria mahiri, uadilifu wa hali ya juu na katika masuala yahusuyo ripoti ya ukaguzi, wanawajibu wa kuhakikisha ushahidi unaendana na vigezo stahiki vya kitaalam vya ukusanyaji wa ushahidi na matakwa ya kisheria”, alisistiza Mganga.

Alisema wanasheria katika baadhi ya taasisi wamekuwa wakihusishwa kikamilifu pale tu masuala mbalimbali yanapoonekana kuharibika jambo ambalo si sahihi lakini wanasheria wa Taasisi Kuu ya Ukaguzi ya Tanzania wao wanashirikishwa kikamilifu katika kaguzi mbalimbali ikiwemo Kaguzi Maalum na Kaguzi za Uchunguzi. “leo hii wanasheria wanapaswa kushiriki kikamilifu katika hatua mbalimbali za ukaguzi ili kupata ripoti za ukaguzi zenye ubora wa kuongeza uwajibikaji. Akifafanua zaidi amesema, wanasheria wa taasisi hizi ndio washauri wa ndani wa masuala ya kisheria hivyo wanapaswa kuwa na uelewa na ujuzi wa kutosha wa masuala ya ukaguzi, kufanya utafiti wa masuala ya sheria, kutoa ushauri wa kisheria katika mikataba na dhamira ya kweli katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Pamoja na changamoto zingine zinazoikabili Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka katika kusimamia kesi mbalimbali zinazowasilishwa, ni kukosekana ushahidi wa kitaalam hivyo aliwataka wanasheria wa taasisi hizo kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika ukaguzi na kusaidia katika masuala yahusuyo sheria.

Naye Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa J. Assad amewashukuru wanasheria kutoka nchi wanachama wa AFROSAI-E kwa kukubali kushiriki katika fursa hii muhimu ya kubadilishana ujuzi wa namna bora ya kuongeza ufanisi katika Ofisi za Taifa za Ukaguzi katika masuala yahusuyo sheria.

Warsha hii ya wanasheria wa Ofisi za Taifa za Ukaguzi Afrika itafanyika kwa siku mbili na inaongozwa na kauli mbiu isemayo “Wajibu wa Wataalam wa Sheria katika Kuongeza Utendaji na Uhuru wa Taasisi Kuu za Ukaguzi, Afrika”.

Kwa taarifa zaidi ya yaliyozungumzwa kwenye warsha hii tafadhali pekua hotuba zilizoambatishwa kwenye taarifa hii Hotuba ya DPP na CAG akimkaribisha Mgeni Rasmi – DPP

2015

Comments are closed.