NAOT

Hotuba ya Katibu Mkuu Kiongozi kwenye hafla ya kumuaga aliyekuwa Mdhibiti Na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Ndugu Ludovick S. L. Utouh, Hyatt Regency Kilimanjaro Hotel, Dar Es Salaam, Tarehe 11 Desemba, 2014

Bw. Ludovick S.L. Utouh,

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (Mstaafu),

Makatibu Wakuu,

Naibu Katibu Mkuu,

Waheshimiwa Viongozi wa Taasisi Mbalimbali,

Ndugu Wanahabari,

Wageni Waalikwa,

Mabibi na Mabwana.

Ninayo furaha na heshima kubwa kukukaribisheni nyote kwenye hafla hii mahsusi ya kumpongeza na kumuaga aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ndugu yetu Ludovick S.L. Utouh, ambaye alistaafu rasmi, na kwa heshima kubwa, kwenye nafasi hii tarehe 19 Septemba 2014, baada ya kuitumikia kwa miaka saba na miezi kumi tangu alipoteuliwa tarehe 19 Agosti, 2006.

Kazi hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ilikuwa kilele cha Utumishi wa Umma wa Bwana Ludovick Utouh ambaye aliwahi pia kuwa Mhadhiri katika kilichokuwa Chuo cha Uongozi wa Maendeleo cha Mzumbe (IDM), na baadaye akawa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA). Kote huko aliacha sifa nzuri ya utendaji, umakini na uadilifu.

Pia, katika hafla hii ya leo, japo hatunaye, tunampongeza na kumkaribisha Profesa Mussa Juma Assad aliyeteuliwa rasmi kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuanzia tarehe 5 Novemba, 2014. Ilikuwa awe nasi leo lakini kutokana na majukumu aliyoachiwa na Ndugu Utouh ya kukagua Umoja wa Mataifa imebidi aende New York kwa mkutano unaohusu majukumu hayo, na akiwa huko atakabidhiwa Uenyekiti wa Bodi ya Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa, jambo linalozidi kupeperusha juu bendera ya taifa letu katika jumuiya ya kimataifa.

Ndugu Viongozi na Wageni,

Siku hii ni siku ya kukumbuka na kumshukuru sana mwenzetu, Ndugu Ludovick Utouh, kwa utumishi wake mrefu uliotukuka, na kwa mambo mengi aliyoyafanya kuimarisha na kuboresha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ya Tanzania kimuundo, kiutendaji na kimaslahi. Hii ni siku pia ya kukumbuka juhudi zake za kufanya kazi kwa uhuru kamili, lakini kwa mahusiano mema na wengine Serikalini.

Ukweli ni kuwa sote, kuanzia kwa Mheshimiwa Rais, na sisi wengine, tungetamani sana Ndugu Utouh aendelee kwenye nafasi hii. Hata hivyo, sheria ni sheria. Kifungu cha 6 (2) (a) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 kinasema kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali lazima astaafu nafasi hiyo anapofikisha umri wa miaka 65. Hatukuwa na la kufanya alipofikia umri huo.

Mchango binafsi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh:

Ndugu Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Bwana Ludovick Utouh atakumbukwa sana kwa mchango wake mkubwa alioutoa ndani ya Ofisi yake, Serikalini kwa ujumla na nje ya nchi. Kutokana na mchango wake huo, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, alimtunuku Nishani ya Utumishi Mrefu na Maadili Mema tarehe 9 Desemba 2012.

Mafanikio haya yote yametokana na uwezo, weledi na bidii katika kufanya kazi na pia kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma. Kwa hakika, Ndugu Utouh anatuachia mfano wa kuigwa na kila aliye katika utumishi wa umma, na mfano huo ni kigezo cha kila mmoja kujipima nacho.

Pengine ni muhimu kwangu kuyabainisha japo mambo machache ambayo Ndugu Ludovick Utouh atakumbukwa nayo.

 1. Ushauri wake kwa Serikali katika kuanzishwa kwa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani (Internal Auditor General);
 2. Ushauri kuhusu kuondolewa kwa Wabunge katika Bodi za Mashirika ya Umma ili kuboresha uwajibikaji na kuepusha mgongano wa kimaslahi;
 3. Mapendekezo ya kuboresha Sheria na miongozo mbalimbali ya Serikali za Mitaa na maeneo mengine;
 4. Ushauri wake kwa Serikali kuhusu kutumia viwango vya uandaaji taarifa za fedha vinavyokubalika kimataifa (IPSAS);
 5. Uanzishwaji wa aina mpya za ukaguzi ndani ya Ofisi ya Ukaguzi kama vile Ukaguzi wa Ufanisi, Ukaguzi wa Mazingira, na Ukaguzi wa Kiuchunguzi;
 6. Kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuwa mshiriki katika Bodi ya Ukaguzi wa Umoja wa Mataifa;
 7. Kujenga mahusiano mazuri kati ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bunge na Serikali. Hali kadhalika, chini ya Uongozi wake, Ofisi imejenga mahusiano mazuri na Ofisi za Wadhibiti na Wakaguzi Wakuu wa Hesabu za Serikali wa nchi mbalimbali;
 8. Kutoa taarifa za ukaguzi kwa wakati kwa mujibu wa Sheria jambo linalowezesha taarifa hizo kuwa na tija.
 9. Kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kupata tuzo ya Taasisi bora za Ukaguzi barani Afrika kwa nchi zinazoongea Kiingereza.

Michango hii imeiletea nchi yetu heshima na sifa kubwa ndani na nje ya nchi hivyo kupelekea kuwa mfano bora wa kuigwa na mataifa mengine.

Mchango wa Serikali katika kuiboresha Ofisi ya CAG:

Ndugu Wageni waalikwa,

Kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Ndugu Utouh yalichangiwa na uamuzi wa dhati wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuimarisha taasisi za utawala bora, maadili na udhibiti, ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. Rais alifanya hivyo kwa kuboresha sheria, kuongeza uhuru wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, kuongeza uwazi wa taarifa za ofisi hiyo, na kuboresha mazingira ya kazi. Nitatoa mifano:

 1. Uanzishwaji wa Sheria ya Ukaguzi wa Umma:
 2. ilitunga Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008 pamoja na kanuni zake za mwaka 2009. Sheria hii iliongeza wigo na uhuru wa Ofisi hii katika kutekeleza majukumu yake Kikatiba.

 3. Kuongezeka kwa Bajeti ya Ofisi ya Ukaguzi:

  Serikali iliboresha utaratibu na mchakato mzima wa kupitisha bajeti ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali uliowezesha bajeti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuongezeka kwa asilimia 306% katika kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka wa fedha wa 2008/9 hadi 2013/14.

 4. Kuboreshwa kwa mazingira ya kufanyia kazi:

  Serikali imeboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi kama ifuatavyo:

  Ujenzi na ukarabati wa majengo ya ofisi katika mikoa ya Shinyanga, Morogoro, Lindi, Kilimanjaro, Mbeya na Singida ikiwa ni pamoja na kuwekewa samani mbalimbali.

  • Kutenga fedha za kujenga majengo mawili kila mwaka wa fedha, hali ambayo imeifanya Ofisi hii kuwa na majengo ya kisasa ya kufanyia kazi zake
  • Kukamilisha jengo la Makao Makuu ya Ofisi huko Dodoma linalotarajiwa kuzinduliwa mapema mwakani.

 5. Ajira na mafunzo kwa wafanyakazi:
 6. Kuanzia mwaka 2008 Serikali imekuwa ikitoa vibali vya kuajiri watumishi wa kada mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya ofisi hii, na kwa lengo la kuimarisha ofisi hii kiutendaji. Pia, watumishi wa Ofisi hii wamekuwa wakipatiwa mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi kupitia fedha ya Serikali na za wafadhili mbalimbali. Kupitia mafunzo haya, kwa sasa ofisi inao wahitimu mbalimbali katika nyanja tofauti kama ifuatavyo:

  • Watumishi 233 wenye sifa za CPA>;
  • CISA (Certified Information Systems Auditor) Watumishi 14;
  • Watumishi 4 wa CFE (Certified Fraud Examiner);
  • Watumishi 11 wenye Certified Procurement and Supplies Professional (CPSP);
  • Aidha watumishi waliobakia wana shahada ya kwanza au shahada ya uzamili ambapo wengine wanajiendeleza katika ngazi mbalimbali za elimu.
 7. Kuridhia Mikataba ya Kimataifa:

  Serikali iliridhia Azimio la Umoja wa Mataifa Na. A/66/209 linalohusu kuwepo kwa ufanisi, uwajibikaji, tija na uwazi katika usimamiaji wa rasilimali za umma kwa kuimarisha Ofisi za Taifa za Ukaguzi tangu Desemba 22, 2011. Hii imesaidia sana Ofisi hii kutambulika na kukubalika kimataifa.

 8. Ukaguzi wa Hesabu za Umoja wa Mataifa:

  Kupitia jitihada kubwa za ushawishi zilizofanywa katika ngazi mbalimbali, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, (UNGA) uliichagua Tanzania kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja huo, kwa kipindi cha miaka sita kuanzia Julai 1, 2012 mpaka Juni 2018. Tangu wakati huo, Ndugu Ludovick Utuoh na timu yake wameiwakilisha kwa ukamilifu nchi yetu, na kwa kweli tunajivunia sana kuwa na watendaji mahiri kama hawa.

 9. Usomaji wa Ripoti za Mdhibiti:

  Kwa mara ya kwanza Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliitisha vikao mbalimbali, kwa nyakati tofauti na Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa kusisitiza umuhimu wa kuzipitia na kuzifanyia kazi taarifa zinazotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Hii imeleta mwamko mpya katika kuona umuhimu wa ripoti hizi na kutumika katika kufanya maamuzi mbalimbali serikalini.

 10. Uundwaji wa Kamati ya Ufuatiliaji wa Mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali:

  Katika kuhakikisha mapendekezo ya CAG yanafanyiwa kazi, Serikali, chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, iliunda Kamati ya Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Mapendekezo yanayotolewa na CAG katika ripoti zake. Kamati hii ni ya kudumu na imesaidia sana kuhakikisha kwamba mapendekezo ya CAG yanafanyiwa kazi kwa wakati, na taarifa kutolewa.

Matokeo ya Mageuzi hayo: Kitaifa na Kimataifa:

Ndugu Wageni waalikwa,

Kutokana na mambo ambayo yamefanywa na Rais Kikwete, na juhudi kubwa iliyofanywa na Ndugu Utouh tunajivunia mafanikio yafuatayo:

 1. Kujulikana kwa Ofisi kitaifa na kimataifa ambapo imeweza kupata kazi za kimataifa na kuwa mwanachama katika taasisi mbalimbali za kimataifa kama vile AFROSAI-E, INTOSAI na nyinginezo.
 2. Kuongezeka kwa uwazi na uwajibikaji wa Serikali katika kuwatumikia wananchi.
 3. Kuwafanya wadau wa maendeleo kuendelea kuiamini serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kazi nyinginezo.
 4. Kuipandisha hadhi Ofisi ya Ukaguzi katika taasisi za kimataifa zinazopima utendaji wa Taasisi za Ukaguzi kutoka ngazi ya kwanza hadi ya tatu kwa ubora.
 5. Taarifa za ukaguzi kuwa na ubora na kuwafikia wadau wengi kwa wakati na kwa lugha rahisi, ikiwemo kupitia tovuti ya ofisi hiyo.
 6. Kufanya aina tofauti za ukaguzi zinazolenga kuboresha utendaji wa Serikali ili kuongeza tija katika mapato, matumizi na ubora wa huduma zinazotolewa.
 7. Kupata tuzo ya kimataifa kuhusu mchango wa Ofisi katika Taasisi ya Kikaguzi ijulikanayo kama ‘AFROSAI-E award’.
 8. Ofisi imeendelea kufanya mikutano yake ya mwaka ambapo imekuwa ikiwaalika wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuboresha tasnia ya ukaguzi.

Tunachoweza na tunachohitaji kujifunza:

Wageni waalikwa,

Kupitia utendaji bora wa Ndugu Ludovick Utouh akiwa kama Mtumishi wa Umma, tunayo mambo mengi ya kujifunza kutoka kwake. Baadhi ya mambo hayo ni kama yafuatayo:-

 

 1. Kuzingatia maadili ya utumishi wa umma wakati wote.
 2. Kujiamini katika utendaji kazi hasa katika kutoa maamuzi na kuyasimamia.
 3. Kujenga ushirikiano baina ya watumishi na taasisi nyingine ndani na nje ya Serikali.
 4. Unyenyekevu kwa viongozi, watumishi na wananchi tunaowatumikia.
 5. Kufanya mambo kwa uwazi na weledi mkubwa
 6. Kufanya kazi kwa bidii na kuwashirikisha waliopo chini yake pasipo ubaguzi na kutetea masilahi ya watumishi.

  Hitimisho:

  Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,

  Kwa yote haya, na mengine mengi, Ndugu yangu Utouh tunakushukuru sana, tutakukumbuka, na tunakutakia kila la kheri. Hali kadhalika, nirudie kumpongeza sana Profesa Mussa Juma Assad kwa kuteuliwa kushika wadhifa huu muhimu katika taifa letu. Aidha, ninamshukuru sana Bwana Francis Mwakapalila kwa kazi nzuri aliyoifanya wakati wa kukaimu nafasi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali tangia Septemba, 2014. Hongera sana.

   

  Shukrani zangu za mwisho, kwa kutajwa, lakini si mwisho kwa umuhimu, ni kwako shemeji yetu, Mama Utouh, kwa uvumilivu mkubwa kipindi chote ambacho mumeo mpenzi alitumikia taifa katika nafasi hii kubwa sana kwenye Utumishi wa Umma. Ukishika nafasi hizi lazima familia iwe na uvumilivu mkubwa. Naungana nawe kumshukuru Mungu kuwa Ndugu Utouh amestaafu kwa heshima na amerejea nyumbani akiwa mzima, buheri wa afya.

  Mama mmoja aliulizwa anaonaje baada ya mume wake kustaafu. Akajibu “Twice as much husband for half the income”. Nina uhakika Ndugu Utouh hatakuwa na “half the income”, lakini atakuwa “twice as much husband”.

   

  Nyote wawili nakutakieni maisha marefu, ya afya njema na furaha tele katika kustaafu ambako Ndugu Utouh anastahili baada ya Utumishi wa Umma uliotukuka na kusifika.

   

  Mungu awabariki sana.

   

  ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.

2014

Comments are closed.