Mwenyekiti wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa (UNBoA) ambaye ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa India Bw. Rajiv Mehrishi ameongoza kikao cha 72 cha Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa.
Akizungumza na wajumbe wa Bodi hiyo baada ya kusaini kwa pamoja ripoti za Ukaguzi za Taasisi za Umoja wa Mataifa, Bw. Mehrishi ameipongeza Tanzania kwa mchango mkubwa aliotoa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi chote cha miaka sita akiwa Mjumbe wa Bodi hiyo.
Naye Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Juma Assad akizungumza na wajumbe wenzake baada ya kuwasilisha ripoti 13 za Ukaguzi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) amesema, Tanzania itaendelea kushirikiana na Bodi hiyo katika kipindi chote cha miaka miwili ambacho ataendelea kuwa Mjumbe Mwangalizi kwenye Jopo la Wakaguzi wa Nje wa Umoja wa Mataifa. Pichani ni Mwenyekiti wa UNBoA Bw. Bw. Rajiv Mehrishi (katikati), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Tanzania Prof. Mussa Juma Assad (kushoto) na Bw. Jorge Bermudez Soto (kulia).