NAOT

NAOT kukagua Umoja wa Mataifa (UN)

Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) imeanza rasmi kukagua Hesabu za Umoja wa mataifa. Ukaguzi huu umeanza rasmi tarehe 01 Julai 2012. Akizungumza na vyombo vya habari leo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo asubuhi katika Ukumbi mkubwa wa mikutano uliopo makao makuu ya NAOT, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) amewataka watanzania kuisaidia ofisi yake kwa taarifa zenye kuongeza ufanisi katika kutekeleza jukumu hili jipya.

Akifafanua ukubwa wa kazi hii alieleza NAOT imepangiwa kukagua mashirika sita (6), mahakama mbili (2) na makundi ya usalama mawili (2) yote ni chini ya umoja wa mataifa.

NAOT ilipokea rasmi jukumu hili kutoka kwa Ofisi ya Ukaguzi ya Afrika Kusini, tarehe 25 Julai 2012 katika hafla iliyofanyika New York, Marekani.

CAG amesema mchakato wa kukagua Umoja wa Mataifa ulianza mwaka 2010 na ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri wa mambo ya nje Mhe. Bernard Membe na aliyekuwa Balozi wa Tanzania Marekani walifanikisha mchakato wa kuuhakikishia Umoja wa Mataifa (UN) kwamba Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali inaweza kutekeleza jukumu hilo.

 

2012

2 responses to “NAOT kukagua Umoja wa Mataifa (UN)”

  1. Eva Mwabulambo says:

    Tuna waamini , fanyeni kweli,tunawaombea.

  2. William Mbwana says:

     Tunatambua mnaenda si kugagua tuu ila kupata uzoefu wa namna ofisi zilizopo chini ya Umoja wa mataifa zinavyoweka hesabu zao. Itawasaidia kuzipa elimu ya utunzaji wa hesabu ofisi za serikali yetu zikiwa ni pamoja na Halmashauri, wizara na nyingine.
    Nawatakia heri na mafanikio, sina wasiwasi na ofisi ya cag. Ninaiamini kwakua imejaa wataalamu wenye weledi wa kazi za mahesabu.