NAOT

PROF. ASSAD AZUNGUMZA NA WATUMISHI WAKE NAMNA YA KUONGEZA UFANISI MAHALI PA KAZI

Katika kuadhimisha wiki ya utumishi wa umma Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Assad Juni 28 mwaka huu ameongea na watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) kutoka Makao Makuu na NAOT Wizara ambao hawapo tawi la Tamata na NHC ili kujadili masuala mbalimbali ya kikazi na changamoto zinazowakabili watumishi wake.

Akizungumza kama mwajiri wao Prof. Assad amewataka viongozi wote wa idara na vitengo vilivyopo ndani ya Ofisi yake wawe mstari wa mbele katika kusimamia maadili ya utumishi wa umma. Aidha, Prof. Assad alisitiza juu ya uchapakazi na uweledi katika kutekeleza majukumu yetu pasipokutegemea zaidi malipo ya posho maalum au posho ya masaa ya ziada kama ilivyokuwa hapo awali.

Alifafanua kuwa kutokana na ufinyu wa bajeti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa mwaka wa Fedha 2016/17 Ofisi haitaweza kugharamia mafunzo ya mara kwa mara yanayohitajika kwa watumishi hivyo ni wakati wa kila mtumishi kuangalia namna gani fursa ndogo zitakazopatikana aidha ataweza kuchangia au kujigharamia yeye mwenyewe kwa faida ya kuongeza ufanisi katika kazi zake.

“Watumishi na viongozi wote wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ni watumishi wa umma ambao wanapaswa kufanyakazi kwa mujibu wa kanuni na sheria za utumishi wa umma. Pia ni muhimu kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii na si bidii tu bali hakikisha kila siku unafanya kazi vizuri zaidi, alisema Prof. Assad. Aliongeza kuwa, tuepuke kubaguana pia kutoa na kupokea rushwa. Natambua NAOT ni taasisi kubwa yenye watumishi 1065 ambao kati ya watumishi 732 ni wakaguzi na 283 ni watumishi wengine. Ofisi hii inapimwa mara kwa mara kwa kuangalia ubora wa kiutendaji ambapo kwenye tathmini ya upimaji inayoendelea inaonesha NAOT imefikia kwenye ngazi ya 3.9 na tunapaswa kufikia ngazi ya 4. Hatuwezi kufikia ngazi hiyo ikiwa mapungufu na changamoto zinazoonekana hazitarekebishwa” alisisitiza Prof. Assad.

 

Prof. Assad pia aliwashukuru watumishi wa Ofisi yake kwa jitahada mbalimbali ambazo zimekuwa zikioneshwa na baadhi ya watumishi wake katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ya kikatiba kwa ufanisi zaidi. Alisema, huwezi kutenganisha mafanikio ya Ofisi na watumishi kwani amaamini mafanikio hayo yametokana na jitihada za watumishi zaidi katika kufanya kazi kwa uadilifu na ueledi wa hali ya juu.

 

Vilevile, Prof. Assad aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusaidia kuboresha mazingira ya uhuru ya ufanyaji kazi wa Ofisi yake ambapo alitaja ni pamoja na kuiwezesha NAOT aidha kujenga majengo yake kama vile katika mikoa ya Manyara, Mbeya, Shinyanga, Singida, Morogoro na Dodoma au kutoa fedha zilizoiwezesha Ofisi yake kulipia pango kwenye mikoa ambayo bado NAOT haijapata umiliki wa majengo yake mwenyewe.

Mwisho liwataka watumishi wote kutumia rasilimali chache zitakazopatikana kwa kuangalia tija, uwekevu na ufanisi.

2016

One response to “PROF. ASSAD AZUNGUMZA NA WATUMISHI WAKE NAMNA YA KUONGEZA UFANISI MAHALI PA KAZI”

  1. EZEKIEL NZUKI says:

    Kazi nzuri sana CAG kafanya ya kuwanoa vijana wake ili waendanae na kasi ya mabadiliko katik kazi zao za kila siku

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *