NAOT

RAIS KIKWETE APOKEA RIPOTI ZA CAG YA UKAGUZI WA MWAKA UNAOISHIA TAREHE 30 JUNI 2014

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amepokea ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa J. Assad  kwa Ukaguzi wa mwaka unaishia tarehe 30 Juni 2014. Prof.  Assad  kwa mara mara ya kwanza, amewasilisha kwa Mhe. Rais Kikwete ripoti za Ukaguzi tangu ateuliwe kushika wadhifa huo wa CAG Novemba 2014. Ripoti hizi zilizo wasilishwa Machi 27 mwaka huu, ni kwa mujibu wa Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo pia ni sanjari na kifungu cha 10 cha Sheria ya Ukaguzi ya Umma ya Mwaka 2008.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hizo, Rais amesema ripoti hizo zitawasilishwa bungeni kwa mujibu wa ibara ya 143 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na mawaziri husika.

Pia, Mhe. Rais ameipongeza sana Ofisi ya CAG kwa mchango wake mkubwa unaoisaidia serikali katika kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa shughuli zake. Vilevile, ameipongeza Ofisi ya CAG kwa uwakilishi mzuri kwenye ukaguzi wa Umoja wa Mataifa (UN Audit). “nimepata habari zenu kuhusu ukaguzi wa umoja wa mataifa na kwa taarifa nilizonazo mnafanya vizuri sana, hongereni kwa kazi nzuri inayoilettea nchi heshima kubwa, alisisitiza Dkt. Kikwete.”

Akielezea baadhi ya mafanikio Mhe. Rais amesema anatambua mchango mkubwa wa Ofisi ya CAG katika kusaidia mapungufu ya mianya inayotumika kuongeza ubadhirifu wa matumizi ya mali za umma.  Akizungumzia matatizo yanayozikabili Halmashauri, Rais amesema kuwa tatizo la watumishi wasio na sifa katika fani ya uhasibu kwenye ngazi ya Halmashauri, serikali imejitahidi kutatua tatizo hilo kwa kuajiri watumishi wa fani ya uhasibu zaidi ya wahasibu 770 wenye sifa  na sasa kuna maboresho makubwa sana katika halmashauri zetu.

Pia amesisitiza kuwa CAG aendelee kuangalia maeneo yote ambayo serikali inaweza kuchukua hatua ili kuondokana na mianya ya upotevu wa rasilimali za umma. Amesisitiza pia katika kipindi chake chote akiwa kama Rais amejaribu kuhakikisha Uhuru wa CAG unazingatiwa kwa kuhakikisha serikali inajenga majengo ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ili wakaguzi wasikae kwenye Ofisi za wakaguliwa.

Naye Prof. Assad akizungumza na Mhe. Rais wakati wa kuwasilisha ripoti yake amemshukuru sana Mhe. Rais kwa ushirikiano anaoutoa kwa Ofisi hii katika kuhakikisha kuwa  Ofisi ya CAG inatekeleza majukumu yake ya kikatiba kwa uhuru na ufanisi wa hali ya juu. Vile vile, ameiomba serikali kuendelea kutekeleza mapendekezo ya CAG ili kuongeza uwajibikaji katika kukusanya na kutumia rasilimali za umma.

Akiipongeza serikali kwa hatua inayochukua katika kutekeleza mapendekezo ya CAG Prof. Assad amesema uanzishwaji wa kamati maalum chini ya uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi  ya kuratibu utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi sanjari na kuundwa kitengo maalum katika ofisi ya mkaguzi Mkuu wa Ndani kinachoshughulika na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo ya CAG ni hatua nzuri sana itakayosaidia kuongeza uwajibikaji.
Ripoti zilizowasilishwa kwa Mhe. Rais ni Ripoti ya Serikali Kuu, Ripoti ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ripoti ya Mashirika ya Umma, Ripoti ya Miradi ya Maendeleo na Ripoti tano za Ufanisi.


2015

Comments are closed.