NAOT

Ripoti ya CAG kwa Mwaka 2014/15 yawasilishwa Bungeni

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni 2015 imewasilishwa leo bungeni. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusomwa kwa ripoti yake Prof. Mussa J. Assad amesema kwa mwaka 2014/15 ametoa jumla ya Hati za Ukaguzi 465 zinazohusu Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma. Kadhalika, ametoa Hati 799 zinazohusu Miradi ya Maendeleo.

Akifafanua kuhusu taarifa ya ukaguzi Prof. Assad amesema masuala yaliyojitokeza kwenye taarifa za ukaguzi wa serikali kuu, serikali za mitaa na miradi ya maendeleo ni pamoja na udhaifu katika usimamizi wa fedha za umma ambapo taarifa za Hesabu zilizokaguliwa zilionyesha upungufu wa fedha zilizopelekwa Serikali Kuu pamoja na Serikali za Mitaa kinyume na bajeti iliyo idhinishwa na Bunge. Fedha za matumizi ya kawaida zilizopokelewa ni Shilingi bilioni 807.65 wakati fedha kwa ajili ya matumizi ya maendeleo zilikuwa Shilingi trilioni 1.82. Aidha, kwa upande wa utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kulikuwa na matumizi ya kiwango kidogo cha fedha. Kwa Serikali Kuu fedha za Miradi ya maendeleo ambazo zilitolewa lakini hazikutumika ni Shilingi bilioni 38.02 sawa na asilimia 1.29 na Shilingi bilioni 101.33 sawa na asilimia 18 kwa Serikali za Mitaa hivyo anaishauri Serikali kuzipatia Taasisi za Serikali fedha za ruzuku kwa Matumizi ya Kawaida na Maendeleo kwa wakati na kwa kiasi kilichoidhinishwa na Bunge ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato ya ndani Prof. Assad amesema mapato yatokanayo na kodi katika mwaka wa fedha 2014/15, ni asilimia 89 ya mapato halisi yaliyokusanywa kutokana na kodi ambapo ni jumla ya shilingi trilioni 10.8 ambapo ikilinganishwa na makisio yaliyopitishwa na Bunge ya shilingi trilioni 12 kuna upungufu wa shilingi trilioni 1.2 sawa na asilimia 11.

Kwa upande mwengine Prof. Assad amesema mapato yasiyotokana na kodi yaliyokusanywa na Serikali Kuu kwa mwaka 2014/15 yalikuwa shilingi bilioni 617 sawa na asilimia 86 dhidi ya makisio ya shilingi bilioni 717, hivyo kutofikia lengo la makusanyo kwa shilingi bilioni 100, sawa na asilimia 14 ya makisio yaliyoidhinishwa na Bunge. Na kwa upande wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2014/15 zilikusanywa Shilingi bilioni 409 sawa na asilimia87 dhidi ya makisio ya shilingi bilioni 471, hivyo kutofikia lengo la makusanyo kwa shilingi bilioni 62 sawa na asilimia13.

Maeneo mengine aliyozungumzia Prof. Assad ni pamoja na Deni la Taifa ameeleza kuwa hadi tarehe 30 Juni, 2015 Deni la Taifa lilikuwa shilingi trilioni 33.54 na katika hili, deni la ndani lilikuwa Shilingi trilioni 7.99 na deni la njeni trilioni 25.55 ambapo ni ongezeko la trilioni 7.05 sawa na asilimia 27 ikilinganishwa na deni la Shilingi trilioni 26.49 lililoripotiwa Juni 30, 2014. “Uchambuzi wangu umeonyesha kuwa malipo ya kugharamia madeni ya kiasi cha Shilingi trilioni 4.60 mwaka huu ni sawa na asilimia 46 ya makusanyo yandani ya Serikali ya Shilingi trilioni 10.8. Gharama hizo zikijumuisha na gharama nyingine kama vile mishahara ya wafanyakazi na likizo, Serikali hubaki na kiasi kidogo cha fedha za kugharamia miradi ya maendeleo na huduma nyingine za kijamii”, alifafanua Prof. Assad.

Masuala mengine yaliyoripotiwa na CAG ni pamoja na mishahara iliyolipwa kwa watumishi ambao hawapo kazini katika Taasisi 16 za Serikali Kuu imeongezeka kutoka Shilingi milioni 141mwaka 2013/14 hadi kufikia Shilingi milioni 393 mwaka 2014/15. Aidha, CAG alifafanua kiasi cha Shilingi milioni 61 kililipwa kwa Taasisi mbalimbali kama makato ya kisheria katika mishahara iliyolipwa kwa watumishi ambao hawapo kazini. Na kwa upande wa Serikali za Mitaa amesema jumla ya Shilingi bilioni 2.7 zililipwa kama mishahara kwa wafanyakazi waliofariki, waliotoroka, kufa na kufukuzwa kazi katika Halmashauri 74 na kiasi cha Shilingi milioni 721 kililipwa kama makato ya kisheria kwa Taasisi kama Mifuko ya Pensheni, Taasisi za Fedha, Bima ya Afya na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa ajili ya wafanyakazi ambao hawapo kazini.

2016

5 responses to “Ripoti ya CAG kwa Mwaka 2014/15 yawasilishwa Bungeni”

 1. Moses Kamaghe says:

  Taarifa haijaonesha kati ya hati 465 za Serikali kuu na 799 za miradi ya maendeleo,nagapi ni hati safi,mashaka na mbaya? Pia taarifa haioneshi Wizara ngapi zimefanya vizuri na zipi hazijafanya vizuri. Pia taarifa za PDF zinagoma kufunguka tunaomba zifanyiwe kazi ili zifunguke ili tupate picha kamili ya kilichotokea

  • Sarah says:

   Asante kwa mrejesho. Tafadhali jaribu kufungua kwa kutumia network tofauti tofauti. Ikiwa tatizo linaendelea unaweza tupatia anuani yako ya barua pepe tukakutumia moja kwa moja kwenye anuani yako

 2. eric samuel says:

  ki ukweli nchi hii inahitaji mabadiliko ya kuanzia viongozi na wafanyakazi wa kawaida,uzalendo ndio nguzo kuu.
  wahusika wote walihusika kuipatisha hasra au upotevu wa hela hizo serikali,tunaomba sheria isimamiwe kuwawajibisha wahusika bila kuangalia cheo wala sura

 3. Useful report although it falls short of analysing the drivers to the widespread inaction to curb misappropriation of funds. We have to understand the social and cultural factors behind this strange behaviour of us Tanzanians.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *