NAOT

TANZANIA KUFANYIWA TATHMINI NA AFROSA-E

Timu ya tahmini kutoka Umoja wa Ofisi za Taifa za Ukaguzi Afrika kwa nchi wananchama wanaozungumza lugha ya kiingereza (AFROSAI-E) umewasili Tanzania ili kupima ufanisi na utendaji wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT).

NAOT inayoongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad imepokea wataalam kutoka nchi ya Canada, Zambia, Kenya, Ghana, Uganda na South Afrika.

Akizungumza na timu ya Tathmini ya AFROSA – E Prof. Assad wakati wa kikao cha ufunguzi, amewahakikishia wataalam hao kupata taarifa zote watakazozihitaji ili kuwawezesha kutekeleza jukumu lao kwa ufanisi na bila kikwazo chochote.

“Ofisi yangu inataarifa ya ujio wenu na nini haswa mngependa kufahamu katika zoezi lenu la upimaji na tathmini ya utendaji wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. Kwa kuwa tumejiandaa kwa zoezi hili ninawaahidi ushirikiano wa asilimia mia moja ili kuhakiki zoezi lenu linakamilika kwa wakati”, alifafanua Prof. Assad.

Wakipokea taarifa hiyo, mratibu wa zoezi hili kutoka AFROSAI – E aliijulisha Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuwa wanashukuru kwa ushirikiano huo na kuahidi kufanya kazi hii kwa ueledi wa hali ya juu ambapo ifikapo Ijumaa watakuwa na rasimu ya ripoti ambayo itawasilishwa kwenye menejimenti kwa mjadala. Aidha katika zoezi hilo ameeleza litahusisha rejea ya machapisho na nyaraka mbalimbali zilizopo kwenye Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Majalada na Nyaraka mbalimbali pamoja na kufanya mahojiano na baadhi ya wakuu wa idara na vitengo ili kupata taarifa zinazohitajika.

Aidha alifafanua kuwa maeneo yatakayoangaliwa yameainishwa katika vigezo vitano (5) vya upimaji ambavyo ni Uhuru wa Kiutendaji na Mfumo wa Kisheria;  Ubora wa Taasisi katika Usimamizi wa Sguhuli zake; Usimamizi wa Rasilimali Watu; Viwango vya Ukaguzi na Taratibu za Kufanya Ukaguzi na kigezo cha mwisho ni Usimamizi na Mahusiano na Wadau.

Zoezi la tathmini ya utendaji wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali limeanza leo tarehe 10 Julai na linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa wiki hii yaani tarehe 14 Julai, 2017.

Timu ya AFROSAI inahusisha wataalam nane (8) ambao ni  kutoka nchi ya Canada (2), Ghana (1), Kenya (1), Zambia (1), Uganda (2) pamoja na AFROSAI-E Sekretariet (1).

2017

Comments are closed.