NAOT

TANZANIA YAPONGEZWA NA BODI YA UKAGUZI YA UMOJA WA MATAIFA

Mwenyekiti wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa (UNBoA) na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa India Bw. Rajiv Mehrishi amemshukuru na kumpongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Prof. Mussa Assad baada ya Tanzania kumaliza muda wake wa kipindi cha miaka sita (6) kuanzia Julai mosi, 2012 cha Ujumbe wa UNBoA na kukabidhi nafasi yake kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Chile Bw. Jorge B. Soto. Pongezi hizo zimetolewa kwenye Kikao cha 72 cha UNBoA kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano uliopo kwenye Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) tarehe 24 Julai, 2018 jijini New York nchini Marekani.

“Ninapenda kuwapongeza sana Tanzania kwa mchango wao mkubwa kwa kipindi chote cha miaka sita (6) waliyotekeleza jukumu hili kubwa na muhimu kwa uweledi wa hali ya juu. Tutaendelea kuutambua na kuenzi mchango huo mkubwa”, alifafanua Mwenyekiti, Bw. Mehrishi.

Pamoja na kufanya makabidhiano hayo, CAG Prof. Assad pia amehudhuria Kikao cha Kawaida cha 72 cha Bodi hiyo na kuwasilisha jumla ya ripoti 13 za Ukaguzi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN).

Akizungumza baada ya kuwasilisha ripoti zake, Prof. Assad amesema kikao hicho ni cha mwisho kwa nchi ya Tanzania kuhudhuria kama Mjumbe wa Bodi ya UNBoA na kinatarajiwa kuhitimishwa kesho tarehe 25 Julai, 2018. Hata hivyo, Prof. Assad amefafanua kuwa Tanzania itaendelea  kuwa mjumbe mwangalizi ”Observer Member” kwenye Jopo la  Wakaguzi wa Nje wa  Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo baada ya kung’atuka kwenye nafasi ya Ujumbe wa Bodi hiyo.

Prof. Assad amesema, katika kipindi cha miaka sita ya UNBoA, Tanzania haikuwa tu Mjumbe wa UNBoA bali pia ilipata fursa ya kuongoza Bodi ya Ukaguzi wa Umoja wa Mataifa (UNBoA) kwa kipindi cha miaka miwili (2).

”Nimekuwa mwenyekiti wa UNBoA kwa miaka miwili mfululizo kuanzia  Januari Mosi, 2015 hadi 31 Desemba, 2016 ambapo nimekuwa na jukumu la kuwasilisha taarifa za UNBoA katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Nilitumia fursa hiyo kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa niaba ya UNBoA njia bora ya kuimarisha mifumo ya udhibiti katika usimamizi wa fedha pamoja na kubadili muda wa uwasilishaji wa hesabu za Mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo yanatoa hesabu zake mwishoni mwa mwezi Aprili”, amesema CAG Prof. Assad.

 Tanzania inaingia katika historia ya dunia kuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na ya tatu (3) Barani Afrika kuteuliwa mjumbe wa Bodi ya Ukaguzi wa Umoja wa Mataifa (UNBoA) tangu kuanzishwa kwa Bodi hiyo mwaka 1946.  Nchi nyingine za Afrika ambazo zimewahi kuwa wajumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa ni Ghana na Afrika ya Kusini tu.

Tanzania imekuwa mjumbe wa Bodi hiyo kuanzia  Julai Mosi, 2012 hadi tarehe 30 Juni, 2018 baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuteuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa mjumbe wa Bodi hiyo mnamo tarehe 11 Novemba, 2011,  kwenye Kikao cha 58 cha Baraza hilo. Tanzania ilishirikiana na wajumbe wengine wa Bodi kutoka nchi za Uingereza, China, Ujerumani na India kwa vipindi tofauti.

 

2018

Comments are closed.