Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imeanza kikao kazi na waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari vinavyotumia mitandao ya kijamii (social media platforms) ili kutoa mafunzo ya siku tatu kwa ajili ya kuwajengea uelewa juu ya utekelezaji wa program ya mapambano endelevu dhidi ya rushwa Tanzania.

Akizungumza katika kikao kazi hicho ambacho kinafanyika chini ya Program ya kujenga uwezo endelevu na kupambana na rushwa Tanzania (BSAAT) na kuhudhuliwa na Mratibu Msaidizi na Ufuatiliaji na Tathmini ya Program hiyo Bwana Josiah Mathew amewataka waandishi hao wa habari kuwa makini na kufuatilia mafunzo hayo huku akiwaeleza umuhimu wa program hiyo kwao wakiwa kama waandishi wa habari ambao kazi yao kubwa ni kuhabarisha na kuelimisha  umma wa Watanzania na dunia nzima kwa ujumla.

Akifungua kikao kazi hicho Mkaguzi Mkuu wa Nje CPAT.  Andindilile Mwabwanga ameeleza  mambo muhimu ambayo wanatakiwa kufahamu katika moja ya mada zitakazowasilishwa kuwa ni kujua mamlaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yani (CAG), Aina na taratibu wa Kaguzi na namna wanavyotakiwa kutoa taarifa zenye viashiria vya udanganyifu na matumizi mabaya ya fedha za umma yanayoibuliwa na ofisi ya CAG.

CPAT. Mwabwanga amewataka waandishi wa habari hao kufanya kazi na ofisi ya Taifa ya Ukaguzi bila kuchoka kwa kuwa wao ni moja ya wadau muhimu katika ofisi hiyo, hivyo ofisi inategegemea ushirikiano mkubwa kutoka kwao ili kuwaelimisha na kuwahabarisha wananchi wapate uelewa juu ya mapato na matumizi ya fedha za umma ambazo ofisi ya CAG ni moja kati ya ofisi zinazotakiwa kusimamia matumizi ya fedha hizo.

Kikao kazi hicho kitamalizika tarehe 14 Januari,2022 kikiwa na lengo kubwa la kuwajengea uelewa wadau wake wakubwa ambao ni waandishi wa habari ambapo ofisi imekuwa ikiwategemea kufikisha taarifa zake kwa wananchi kwa kutumia vyombo vya habari.