Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inaendesha mafunzo ya siku tatu kwa kamati za Bunge, kamati hizo ni; Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) na kamati nyingine za Bunge.

Lengo kuu la kufanya mafunzo haya ni:

  1. Kujenga uwezo wa Waheshimiwa Wabunge kuelewa na kuchambua ripoti za ukaguzi ikiwa ni pamoja na kutumia ripoti za CAG kuhoji Maafisa Masuuli;
  2. Kuimarisha mahusiano na ushirikiano kati ya CAG na Bunge katika

Kuboresha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma.

Akifungua mafunzo hayo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Charles E. Kichere alisema,angependa kuwajulisha Waheshimiwa Wabunge kuwa mafunzo yaliyotolewa ni mwanzo tu wa kujengeana uwezo wa kutumia ripoti za CAG katika kuhoji na kuishauri Serikali.

CAG alibainisha kuwa Mafunzo yatakuwa endelevu kwa kuwa pamoja na kupatiwa ripoti za CAG Bungeni, itawabidi kupata nafasi ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa ili waweze kujionea na kutoa ushauri. CAG alieleza kuwa Serikali inatekeleza miradi mingi kwa kutumia fedha za umma ambazo zinapitishwa na Bunge kila mwaka katika bajeti. Ipo miradi ambayo imetekelezwa vizuri na mingine ambayo utekelezaji wake unakabiliwa na changamoto mbalimbali. Hivyo watakapopata mafunzo juu ya ukaguzi wa miradi watakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa ushauri wenye tija.

Aliongeza kuwa yeye binafsi na Ofisi yake wapo tayari kupokea ushauri wa Waheshimiwa Wabunge na kuufanyia kazi.

Alimaliza kwa kueleza kuwa matumizi ya rasilimali za umma ni suala mtambuka linalogusa kila sekta hivyo basi inampasa kila mmoja wetu kutunza rasilimali za umma.