Mdhibiti  na Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali(CAG), Ludovick Utouh, amesema kuna umuhimu wa kuwapo kwa uwazi na uwajibikaji pamoja na kuwashirikisha wananchi katika mchakato wa ukaguzi wa fedha za umma.

CAG aliyasema hayo jana wakati akifungua warsha ya siku mbili  yenye lengo  la kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani na baadhi ya viongozi wa kamati za bunge na kuongeza kuhusu ushirikishwaji wananchi katika suala zima la ukaguzi wa fedha za umma.

Alisema wananchi wanapaswa kuleta hoja ya suala zima linalohusu ukaguzi wa fedha zao kupitia mashirika ya kiraia na vyombo vya habari.

Aliongeza kuwa ili kuboresha  utawala bora na matumizi sahihi ya rasilimali hizo ni vyema kuwepo na uwazi ili wananchi wawe na taarifa  hiyo bila kificho chochote.

Makamu mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya Hesabu za serikali za  mitaa LAAC(),Seleman Zedi,alisema mafunzo hayo yatawasaidia kupata uwezo wa kushirikisha wananchi katika usimamizi wa ukaguzi wa fedha zao.

Alisema suala la utoaji wa taarifa kwa wananchi kuhusu mapato linahitaji mbinu mbalimbali zilizo sahihi kwa lengo la kuboresha utawala bora.

Aliongeza kuwa uwazi katika taarifa ni jambo linalozidisha imani kwa wananchi, hivyo kupitia kwa wataalam hao wa ukaguzi kutoka katika mataifa mengine ni wazi mabadiliko yataonekana.