Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Ludovick S. L. Utouh, ziliwasilishwa bungeni tarehe 11 Aprili 2013. Ripoti hizi ni za ukaguzi wa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2012. Kwa mujibu wa ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (iliyorekebishwa mara kwa mara) na kifungu cha 34 (2) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008, CAG anatakiwa angalau mara moja kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hesabu zinazosimamiwa na watumishi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Hesabu zinazosimamiwa na Katibu wa Bunge.

Chini ya Ibara ya 143 (4) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CAG anatakiwa kuwasilisha kwa Rais kila ripoti anayotoa chini ya ibara ya 143 (2) ambaye anatakiwa awaagize mawaziri wanaohusika waziwasilishe ripoti hizo mbele ya kikao cha kwanza cha bunge ndani ya siku saba baada ya kuanza kwa kikao.

Kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia (2007/2008), jamii imeshuhudia maboresho katika mchakato wa uwajibikaji nchini. Maboresho haya yametokana na dhamira ya dhati ya Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kamati zake za kudumu ambazo zimesimamia na kuhimiza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.

Katika masuala yaliyojitokeza katika ukaguzi wa mwaka 2011/12 ni pamoja na ukiukwaji wa sheria, taratibu, kanuni mbalimbali, pamoja na udhaifu katika mifumo ya udhibiti wa ndani. Wajibu wa kuhakikisha kuna mifumo thabiti ya udhibiti wa ndani ni jukumu la Maafisa Masuuli.

Ili kukidhi matarajio ya Umma wa watanzania kwa mapana zaidi Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) imeendelea kufanya uchambuzi wa njia bora zaidi za kufanya ukaguzi na kuongeza wigo wa masuala yanayokaguliwa na hivyo kuimarisha utendaji wa uwajibikaji katika sekta ya umma.

Katika ripoti za ukaguzi zilizowasilishwa bungeni mwezi Aprili, 2013, CAG amewasilisha ripoti za ukaguzi wa ufanisi ambazo ni Ripoti ya Usimamizi wa Ukaguzi wa Magari na Mipaka ya Mwendo Kasi Barabarani, Ripoti ya Usimamizi wa Mikataba ya Miradi ya Ujenzi katika Serikali za Mitaa, Ripoti ya Usimamizi wa Uvuvi katika Ziwa Victoria, Ripoti ya Ukaguzi wa Usimamizi wa Usalama Mahali pa Kazi na Ripoti ya Usimamizi wa Manunuzi ya vifaa  vya TEHAMA katika sekta ya Umma. Ukaguzi huu wa ufanisi umelenga kuangalia iwapo rasilimali zilizotolewa zimetumika vizuri ili kuleta matokeo yaliyotarajiwa kwa kuzingatia uwekevu, tija na ufanisi.

Iwapo ripoti hizi zitasomwa kwa undani na kufanyiwa kazi na serikali zitasaidia kwa kiasi kikubwa serikali kujipanda vyema kwa lengo la kuboresha utendaji na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma na hivyo kutimiza malengo na vipaumbele ambavyo serikali imejiwekea.

Kwa maelezo zaidi kuhusu Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zilizowasilishwa kwa Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 28 Machi, 2013 na baadaye kusomwa bungeni na mawaziri husika tarehe 11 Aprili, 2013 zinapatika kwenye tovuti hii www.nao.go.tz