Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Ludovick Utouh amewasilisha ripoti  za ukaguzi wa hesabu za serikali  za mwaka wa fedha 2012/13 kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 28 Machi 2014, Ikulu, Dar es salaam. Ripoti zilizowasilishwa kwa Rais zilikuwa tano kama ifuatavyo:

  1. Ripoti kuhusu Ukaguzi wa Hesabu za Mamlaka za Serikali Kuu
  2. Ripoti kuhusu Ukaguzi wa Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa
  3. Ripoti kuhusu Ukaguzi wa Hesabu za Mashirika ya Umma
  4. Ripoti kuhusu Ukaguzi wa Hesabu za Miradi mbali mbali
  5. Ripoti  Jumuifu ya Kaguzi Sita za Ufanisi (Ukaguzi wa Thamani ya Fedha)

Ripoti hizi zimewasilishwa kwa Rais kulingana na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (kama ilivyorekebishwa mara kwa mara), Ibara ya 143 Ibara ndogo ya 4 ambayo inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwasilisha ripoti zake za ukaguzi kwa Rais. Katiba hiyo hiyo inatamka ya kuwa Rais atahakikisha ripoti hizo zimewasilishwa katika kikao cha Bunge kitakachofanyika baada ya Rais kupokea ripoti hizo kabla ya kupita siku saba tangu siku ya kwanza ya kikao hicho.

Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zitakuwa wazi kwa matumizi ya umma mara zitakapowasilishwa bungeni. Ripoti zilizowasilishwa kwa Rais tarehe 28 Machi, 2014 zitawasilishwa kwenye kikao cha Bunge kitakachokaa mwezi Mei mwaka huu baada ya kukamilika au kuahirishwa kwa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea hivi sasa.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa mstari wa mbele kufuatilia na kutekeleza mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika kuboresha na kuimarisha uwajibikaji wa ukusanyaji na matumizi ya fedha na rasilimali nyingine za umma. Mifano michache ya utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni:

  • Uanzishwaji wa Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani – Wizara ya Fedha
  • Uimarishaji wa Idara ya Msajili wa Hazina
  • Utumiaji wa viwango vya uhasibu vya kimataifa
  • Tathmini ya ubora wa mfumo wa IFMS Epicor
  • Uboreshaji wa sheria mbali mbali za nchi zinazohusu masuala ya fedha

Hata hivyo uwasilishaji wa ripoti ya CAG bungeni kuanzia mwaka 2011 umekuwa na msisimko mkubwa ambapo jamii kwa ujumla wameshuhudia mabadiliko makubwa ikiwemo kuongezeka kwa uwajibikaji kwa viongozi serikali.

Hii imetokana na ufuatiliaji thabiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tazania ambapo limekuwa likitumia ripoti za CAG ipasavyo kuiwajibisha serikali. Makundi mbalimbali kama vile Wafadhili (Development Partners), Asasi za kijamii (CSOs) na Taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) pia zimekuwa zikitumia ripoti za CAG kuelimisha umma na kuhimiza uwajibikaji kwa viongozi na watumishi wa serikali.

Mafanikio haya yametokana na harakati mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa uhuru wa  Ofisi  uliotokana na  Bunge kupitisha  Sheria ya Ukaguzi ya Umma Na. 11 ya mwaka 2008 ambayo imewezesha  kuboresha mchakato wa bajeti ya ofisi  na kuifanya Ofisi  iweze kutekeleza majukumu yake katika mazingira ya uwazi na uwajibikaji. Miongoni mwa mambo yaliyosaidia ubora wa ripoti ya CAG ni kuwepo kwa nia thabiti na mikakati iliyotekelezwa ikiwa ni sambamba na kuendesha mafunzo yenye lengo la kukuza uelewa wa masuala ya ukaguzi kwa wadau mbalimbali kama vile Kamati za Bunge zinazohusika moja kwa moja na bajeti ya serikali au ripoti za CAG, Asasi za Kiraia (CSOs) na Taasisi  zisizo za kiserikali (NGOs). Pia, kumekuwepo na ushirikiano wa kikazi wa karibu sana kati ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi na taasisi za serikali kama Mkurugenzi wa Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa pamoja na Mkuu wa Polisi kulingana na marekebisho yaliyofanywa kwenye kifungu cha 27 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma.

Vilevile, mikakati mbalimbali ya kusambaza taarifa za CAG kwa Umma imekuwa ikitekelezwa ambapo mwaka 2013 kwa mara ya kwanza Ofisi ilifanikiwa kuchapisha na kuzindua toleo maalum la muhtasari wa ripoti za CAG (The CAG Citizen Report ), kitabu kilichohusisha Ukaguzi wa fedha na Ukaguzi wa Uchunguzi. Kwa kuwa lengo la kitabu hiki ilikuwa kumfikia kila mwananchi ilimradi anajua tu kusoma na kuandika lugha ya kiswahili, kitabu hiki kiliandaliwa kwa lugha rahisi na nyepesi sanjari na matumizi ya picha za katuni kwa madhumuni ya kutoa ufafanuzi wa kina kwa maelezo yaliyopo ndani ya kitabu hicho. Kupitia toleo hilo wengi wameonesha kuridhika na mbinu hiyo hivyo kiasi kwamba maombi ya nakala za kitabu hicho kuongezeka zaidi ya makadirio ya awali.

Hata hivyo kwa mwaka huu juhudi za kuongeza nakala pamoja na kukitangaza kitabu hicho kwa njia za Radio na Televisheni zinafanyika ili kuhakikisha kinawafikia  wananchi wengi kwa kadiri ya bajeti itakavyoruhusu na hivyo kufikia lengo la ofisi iliyojiwekea katika kuhimiza uwazi na uwajibikaji katika kukusanya na kutumia fedha za umma.

Katika kuhakikisha ripoti za ukaguzi zinawafikia wadau wetu  kwa haraka na urahisi, Ofisi huwa inaziweka ripoti zake za ukaguzi kwenye tovuti www.nao.go.tz,  mara tu baada ya ripoti hizo kuwasilishwa bungeni.

Vilevile, mara baada ya ripoti kuwasilishwa bungeni, CAG  hufanya mkutano na waandishi wa habari ili kueleza kwa muhtasari mambo muhimu yaliyojitokeza kwenye ukaguzi wa mwaka husika. Baada ya hapo ofisi inakuwa na programu mbalimbali kwa ajili ya kujadili ripoti  za CAG na kutolea ufafanuzi  masuala mbalimbali yatakayojitokeza  kuhusiana na kaguzi hizo.

Endelea kutembelea tovuti ya ofisi  kwa taarifa kamili ya ripoti za ukaguzi wa hesabu za serikali ili ujue kodi yako imetumikaje.