Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Ludovick Utouh amependekezwa na kupitishwa kwa kauli Moja kuwa Mjumbe wa Bodi ya wakaguzi wa Hesabu za Umoja wa Mataifa.

Bw. Utouh amepitishwa na wajumbe wa Kamati ya Tano ya Utawala na Fedha ya Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, katika kikao chake kilichofanyika siku ya Ijumaa, hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Jijini New York, Marekani. Utouh atakuwa mjumbe wa Bodi hiyo kwa kipindi cha miaka sita kuanzia Julai Mosi 2012 akichukua nafasi itakayoachwa wazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Afrika ya Kusini anayemaliza muda wake mwezi Juni mwakani.

Tanzania inakuwa nchi ya tatu kutoka Afrika kuingia katika Bodi hiyo tangu ilipoanzishwa. Nchi nyingine kutoka Afrika ambazo zimewahi kuwa wajumbe wa bodi ni Ghana na Afrika ya Kusini.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Seriakali atafanya kazi na wajumbe wengine wawili ambao pia ni wadhibiti na wakaguzi wa hesabu kutoka Serikali za China na Uingereza, baadhi ya majukumu ya Bodi ya wakaguzi wa hesabu za Umoja wa Mataifa, ni pamoja na kukagua Vitabu vya hesabu za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Mashirika na asasi zote zilizochini ya Umoja wa Mataifa , Misheni za ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa, miradi mbalimbali inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa, hesabu za Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai zikiwamo za mauaji ya kimbari ( Rwanda na Yugoslavia)

Bodi hiyo hukutana mara mbili kwa mwaka katika miezi ya Juni na Novemba. Pamoja na kwamba wajumbe wa bodi hiyo hutakiwa kukutana mara mbili kwa mwaka, lakini wanaweza kukutana wakati wowote pale wanapohitajika.

Kwa mujibu wa taratibu za kazi, wajumbe hao watatu wa bodi ya wakaguzi wa hesabu za Umoja wa Mataifa ( Tanzania, China na Uingereza) watasaidiwa na wakurugenzi watatu kutoka katika nchi hizo.

Wakurugenzi hao ambao watatakiwa kuwapo muda wote , Ofisi zao za kudumu kwa kipindi hicho cha miaka sita zitakuwa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.