Katika kipindi cha miaka sita iliyopita (2006 hadi sasa) Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) chini ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (CAG), Bw. Ludovick Utouh, kumekuwa na mafanikio makubwa katika uimarishaji wa mawasiliano kati ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi na wadau wa Ofisi hii. Uimarishaji wa mawasiliano umesaidia kuongeza uwajibikaji katika kukusanya na kutumia rasilimali za umma.

Hivi karibuni kumekuwa na warsha na mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo wadau wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali. Kila mwaka mwezi Mei, NAOT imekuwa ikiandaa Warsha maalum (siku mbili hadi tatu ) ya kujadili Uwajibikaji. Warsha hii imekuwa ikihusisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na wataalam wa ukaguzi kutoka taasisi binafsi za ukaguzi zinazokubalika kimataifa, Kamati za bunge zinazosimamia ripoti za CAG, Asasi zisizo za kiserikali, Waandishi wa Habari, Wakaguzi Wakuu kutoka nchi mbalimbali, Watendaji wa Kuu wa Wizara, Taasisi, Idara zinazojitegemea na wa wakilishi kutoka Benki ya Dunia. Hii imesaidia kukuza uelewa masuala ya ukaguzi wa hesabu za serikali sanjari na kuimarisha utawala bora, uwazi na uwajibikaji.

Hizo ni miongoni mwa sababu zilizopelekea Tanzania kuteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya Ukaguzi wa Umoja wa Mataifa (UN). Kuteuliwa kwa Bw. Ludovick S. L. Utouh, ambaye ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuingia kwenye bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa (United Nations Board of Audit – UNBoA), ni heshima kubwa sio tu kwa nchi ya Tanzania bali ni kwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, lakini pia kwa Watanzania wote. Nafasi ya kuwa mjumbe wa UNBoA  ni nafasi iliyokuwa ikishindaniwa na nchi zote duniani ambazo ni wananchama wa Umoja wa Mataifa (UN). Haikuwa kazi rahisi kwa nchi ya Tanzania kupendekezwa na kupitishwa kwa kauli moja kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakaguzi wa Hesabu za Umoja wa Mataifa (UN). Kupata nafasi ya kukagua Umoja wa Mataifa (UN) ni mafanikio makubwa sana kwa nchi na Ofisi yetu.

Kwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT), uteuzi huo ni ushahidi tosha kuwa miongoni mwa watu wenye uwezo mzuri wa kiutendaji duniani, hususani katika ukaguzi wa hesabu za serikali, yupo Mtanzania mwenzetu, Bw. Ludovick S. L. Utouh, ambaye sisi ni mtendaji mkuu wa taasisi yetu lakini kwa kuweka mbele utaifa wetu, tunajiona kuwa na kila sababu ya kujivunia mafanikio yake, ambayo kimsingi ni mafanikio ya nchi nzima.

Bw. Utouh atakuwa mjumbe wa bodi hiyo ya UN, kwa kipindi cha miaka sita kuanzia Julai Mosi, 2012 na atafanya kazi na wajumbe wengine wawili ambao pia ni wadhibiti na wakaguzi wa hesabu kutoka Serikali za China. Kwa uteuzi huo Tanzania inakuwa nchi ya tatu kutoka Afrika kuingia katika bodi hiyo tangu ilipoanzishwa, nchi nyingine kutoka Afrika ambazo zimewahi kuwa wajumbe wa bodi ni Ghana na Afrika ya Kusini.

Baadhi ya majukumu ya bodi hiyo ni kufanya ukaguzi wa hesabu za makao makuu ya UN, mashirika na asasi zote zilizo chini ya UN ambazo ni Misheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa, miradi mbalimbali inayosimamiwa na UN, hesabu za Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai zikiwamo za mauaji ya kimbari za Rwanda na Yugoslavia. Majukumu yote haya na mengineyo mengi yanatoa heshima kubwa kwa Tanzania yetu na kwamba pamoja na umaskini wetu, bado wapo Watanzania wachache ambao kwa jitihada zao binafsi, wameweza kuwafanya watendaji wengine wanaowazunguka katika ofisi zao, wamejikuta wakifanya kazi nzuri hata kuaminiwa kupewa majukumu makubwa zaidi yenye hadhi na uzito huo wa kimataifa.

Sanjari na uteuzi wa kuwa mjumbe wa UNBoA, Bw. Ludovick S. L. Utouh ni miongoni mwa viongozi wa kitaifa waliotunukiwa na Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete  nishani ya Utumishi wa Umma Uliotukuka (Utumishi wa Umma wa muda mrefu na Maadili mema kazini) . Nishani hii alitunukiwa tarehe 9 Desemba 2012 katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya miaka 51 ya uhuru. Nishani hii ni kutokana matokeo ya kazi nzuri ya ukaguzi iliyochangia uimarishaji wa utawala bora na uwajibikaji katika kukusanya na kutumia rasilimali za umma.

Tunachukua fursa hii kumpongeza Bw. Ludovicl S. L. Utouh, kwa kuteuliwa kuwa mjumbe wa bodi hiyo yenye wajibu mkubwa kimataifa, hasa tukitilia maanani uzito na hadhi ya majukumu ambayo yeye na wajumbe wenzake wa Bodi hiyo ya UN watakuwa wakiyasimamia.

Bw. Utouh ni kiongozi mchapakazi, jasiri katika kusimamia ukweli, mwenye kujali watumishi wa ngazi zote, anayeongoza kwa mfano na anayetekeleza wajibu wake kwa kuzingatia maadili ya taaluma na matakwa ya kisheria.

Tunakutakia kazi njema, afya tele unapojipanga kutekeleza majukumu yako ya kikatiba ikiwa ni pamoja na kaguzi maalum za mwaka 2012/13. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick S. L. Utouh katika mwaka wa fedha wa 2012/2013 miongoni mwa kaguzi maalumu anatarajia kufanya ukaguzi wa misamaha ya kodi. Lengo la kufanya ukaguzi huo ni kuangalia kama misamaha inayotolewa imezingatia taratibu za kisheria, kuangalia manufaa katika misamaha hiyo kwa kuzingatia uwekezaji na uchumi wa taifa.

Ukaguzi huo utasaidia kufahamu kiasi cha fedha tunachopoteza katika misamaha ya kodi, kuangalia kama kuna ulazima wa kuendelea kuwa nayo yote jinsi ilivyo na kutoa ushauri wa kitaalamu.