Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh, akizungumza na waandishi wa habari juu ya ripoti ya ukaguzi maalum katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na matumizi ya matengenezo ya magari ya serikali aliyoiwasilisha bungeni Dodoma jana.PICHA: SELEMANI MPOCHI)

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amegundua madudu katika kaguzi nne alizozifanya ikiwemo ubadhirifu wa zaidi ya Sh. bilioni 6.7 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini Dodoma jana, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu na Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, alisema katika ukaguzi huo maalum ulibaini matukio 14 yenye jumla ya Sh. 6,725,694,257 ambayo yana kila dalili za ubadhirifu.

Utouh alisema katika ukaguzi huo maalum wa halmashauri ya wilaya hiyo umeonyesha udhaifu mkubwa uliopo katika mfumo wa udhibiti wa ndani pamoja na ukosefu wa uaminifu wa watendaji kazi.

Utouh alisema katika ukaguzi wa matengenezo ya magari ya serikali, Wizara ya Ujenzi yenye dhamana ya kusimamia magari ya serikali, haina sera ya matengenezo ya magari hali inayosababisha upungufu wa miongozo ya usimamizi wa matengenezo ya gari za serikali.

Pia alisema wamegundua kuwa matengenezo ya magari ya serikali hayasimamiwi kwa ufanisi  na hiyo inasababishwa na kutofanyika kwa ukaguzi baada ya matengenezo iwapo magari yametengenezwa kwenye gereji binafsi.

Utouh alisema ukaguzi wa mapato ya halmashauri yanayokusanywa na wakala chini ya ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), umegundua kuwa mchakato unaotumika kuwapata mawakala wa kukusanya mapato hayo hauna tija.

‘Ushindani ni mdogo na pia vigezo vya tathmini ya zabuni havipo wazi,” alisema na kuongeza kuwa mikataba haiandaliwi kwa nia ya kulinda maslahi ya halmashauri.

UPOTEVU WA MAJI MIJINI

Alisema wizara, mamlaka ya maji na mamlaka za udhibiti hazijachukua hatua sahihi za kukabiliana na tatizo hilo.

Alishauri mamlaka ya maji kuweka kumbukumbu juu ya uvunaji wa maji na kuandaa mipango mikakati ya kuhakikisha kuwa uvujaji wowote wa maji unadhibitiwa ndani ya saa 24 hususan matukio yanayotokea baada ya saa za kazi, mwishoni mwa wiki na siku za sikukuu.

Utouh alisema walifanya ukaguzi katika mapato ya uvunaji wa misitu chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kugundua na kugundua kuwa asilimia nne ya misitu imetayarisha mipango ya usimamizi wa misitu na iliyobaki asilimia 96 inafanya kazi bila kuwa na mipango.

Pia waligundua kuwa wizara haina utaratibu mzuri wa kudhibiti utoaji wa leseni katika wilaya na kamati za uvunaji misitu za wilaya haziripoti kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, maamuzi yaliyofanywa katika mikutano yao ya kujadili maombi ya uvunaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Augustine Mrema, alisema wahusika wa ubadhirifu wa fedha za serikali wamekuwa wakikaa katika vituo vya kazi kwa muda mrefu bila kuchukuliwa hatua licha ya tuhuma zinazowakabili.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Kabwe Zitto, alimuomba CAG kama inawezekana kuharakisha ripoti ya ukaguzi ya  Shirika la Usafiri  la Dar es Salaam (UDA).