Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bwana Charles Kichere amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa J. Assad ambaye amemaliza muda wake.

Katika hafla hiyo ya makabidhiano iliyofanyika katika Jengo la Ukaguzi Jijini Dar Es Salaam, Prof Mussa Assad alianza kwa kumkaribisha Bwana Kichere na kumtaka kufanya kazi kwa ushirikiano na watumishi waliopo kwasababu kazi kubwa ya ukaguzi inafanywa na wao.

“Ujengaji wa uwezo kwa watumishi kwa kushirikiana na taasisi za nje ya nchi ni muhimu sana. Zipo taasisi nyingi za nje ya nchi ambazo hutuletea wataalam mbalimbali kwaajili ya kuwajengea uwezo watumishi, suala la kuwajengea uwezo watumishi likifanyika kikamilifu husaidia katika utendaji kazi mzuri na kujenga jina la taasisi’’ alisema Prof Assad, pia aliahidi kumpatia ushirikiano mkubwa CAG wa pale inapohitajika.

Katika makabidhiano hayo CAG Bwana Kichere alikabidhiwa Sheria ya Ukaguzi pamoja na sera ya Utawala na Rasilimali watu.

Aidha CAG Kichere alishukuru kwa mapokezi na makabidhiano mazuri na kuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kulinda mapato ya serikali. Kazi yangu kubwa ni kulinda kihenge cha Watanzania,ninaahidi kukilinda kwa wivu na kukemea matumizi mabaya ya fedha za Watanzania alisema CAG Bwana Kichere.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliapishwa jana na Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar Es Salaam.