Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mr. Ludovick S. L. Utouh amewasilisha bungeni Ripoti za Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha unaoishia Juni 30, 2010 na Ripoti za Ukaguzi wa Ufanisi na Utambuzi.

Ripoti hizi zilizowasilishwa bungeni tarehe 12 Aprili 2011, ziliwasilishwa kwa Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 29 Machi 2011 ikiwa ni ndani ya muda uliowekwa kisheria kwa mujibu wa ibara ya 143 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (iliyorekebishwa 2005) pamoja na kifungu cha 28 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008.

Ripoti zilizowasilishwa ni matokeo ya ukaguzi wa taarifa za fedha pamoja na ukaguzi wa ufanisi wa kipindi cha mwaka 2009/2010.

Katika ripoti za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Kuu (MDAs 2009/2010) matokeo ya ukaguzi yanaonesha kuwa kumekuwepo na mapungufu kidogo ya ubora wa hati zilizotolewa kwa Serikali Kuu na Taasisi zake ikilinganishwa na mwaka uliopita yaani 2008/2009. Hati za kuridhisha zimepungua kutoka asilimia 87 hadi 77, wakati hati zenye shaka zimeongezeka kutoka asilimia 10 hadi asilimia 21. Matokeo ya ukaguzi kwa mwaka huu yametoa hati 2 zisizoridhisha ikilinganishwa na hati 3 zilizotolewa mwaka 2008/2009 na kwa mwaka huu kuna hati mbaya moja ambapo mwaka jana hati ya aina hiyo haikuwepo. Hati hii imetokana na jengo la Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuungua na hivyo kusababisha hesabu zake kutokuwa kamilifu.

Ukaguzi wa Serikali kuu kwa kipindi kilichoishia tarehe 30 Juni 2010 pamoja na mambo mengine ulichunguza kwa undani juu ya Usimamizi wa Sheria za Fedha za Umma ya mwaka 2001 na Usimamizi wa Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004, Utunzaji wa Vifaa na Mali, Uwekaji Mbovu wa Kumbukumbu na Ukosefu wa Nyaraka na Hati za Malipo, Ukaguzi wa Hazina uliangalia Deni la Taifa, Matumizi ya Serikali, Misaaada kutoka kwa Wafadhili, Matoleo ya Ziada (Overdraft), Dhamana za Serikali, Madeni ya Serikali, Mali za Serikali ambazo hazipo kwenye leja, Fidia kwa waathirika wa hali mbaya ya uchumi, Ukaguzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ulijikita katika Masuala ya Ukaguzi wa miaka ya nyuma, Makusanyo ya Maduhuli na Misamaha ya Kodi. Vilevile ukaguzi uliangalia ukusanyaji wa Maduhuli katika Sekta isiyo rasmi.

Katika ripoti za ukaguzi wa Hesabu za Serikali za Mitaa kwa mwaka 2009/2010 matokeo ya ukaguzi yameonesha kiwango cha utayarishaji wa hesabu za Serikali za Mitaa kimeshuka ikilinganishwa na hesabu zilizotayarishwa mwaka 2008/2009. Kushuka huku nipamoja na sababu nyingine kuchangiwa na Halmashauri kutokuwa na usimamizi na ufuatiliaji wa karibu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa katika ngazi za chini za Serikali yaani kata na vijiji, Ongezeko la fedha zinazohamishwa na Halmashauri kwenda katika ngazi za vijiji na kata chini ya utaratibu wa ugatuaji wa mamlaka kwa wananchi (D by D). Utaratibu huu unahitaji kuwepo uwezeshaji kwa njia ya mafunzo katika usimamizi wa miradi, utunzaji wa fedha na uandaaji wa hesabu. Vilevile, Halmashauri kutozingatia kuimarisha mfumo wa udhibiti wa ndani. Hii ikiwa nipamoja na kuwa na vitengo vya ukaguzi wa ndani vilivyodhaifu, vitengo vya manunuzi visivyomadhubuti, Kamati za Ukaguzi kutofanya vikao vya kutathimini utendaji wa Halmashauri na hivyo kutozishauri menejimenti za Halmashauri.

Ukaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kipindi kilichoishia tarehe 30 Juni 2010 pamoja na mambo mengine ulichunguza kwa undani juu Matumizi yasiyokuwa na hati za malipo, Ruzuku ya Miradi ya Maendeleo isiyotumika, Malipo yaliyokuwa na nyaraka pungufu, Mishahara iliyolipwa isivyostahili, Vitabu vya Risisti ambavyo havikuuonekana, Mapato ambayo hayakuwasilishwa kwenye Halmashauri, Mambo yaliyojitokeza kwenye kaguzi maalu na Mikopo ya Watumishi.

Katika ripoti za Ukaguzi wa Mashirika ya Umma na Taasisi nyinginezo matokeo ya ukaguzi yameonesha kati ya mashirika 170 ambayo yalitegemewa kuwasilisha hesabu zake kwa ukaguzi ni kaguzi za mashirika 122 kati ya 170 sawa na asilimia 71.7 zikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo Mdhiniti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alikamilisha kaguzi 51 tu. Katika Ukaguzi wa Mwaka huu asilimia 75 ya Mashirika yalipata hati safi ikilinganishwa na asilimia 88 ya mwaka jana ikiwa ni upungufu kwa asilimia 13. Kwa upande mwingine, Mashirika yaliyopata hati zenye shaka mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana ni sawa na asilimia 8. Pia, mwaka huu mashirika saba sawa na asilimia 6 yalipata hati zenye shaka na msisitizo, wakati shirika moja limepata hati mbaya.

Ukaguzi wa Mashirika ya Umma na Taasisi nyinginezo kwa kipindi kilichoishia tarehe 30 Juni 2010 pamoja na mambo mengine ulichunguza kwa undani juu Uamuzi wa kutoza ada ya maridhiano (Concesion Fee), Hati miliki za mali za mashirika, Wabunge kuwa wajumbe katika Bodi za Wakurugenzi za Mashirika ya Umma, Ucheleweshaji wa utekelezaji wa Mradi wa Vitambulisho vya Taifa, Ulipaji ada na marupurupu ya wakurugenzi wa Bodi za mashirika ya Umma, Kutotekeleza Waraka wa Msajili wa Hazina, Ucheleweshaji wa utoaji fedha za mikopo kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Utekelezaji wa Mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali.

Katika ripoti za ukaguzi wa ufanisi zilizowasilishwa na kutolewa taarifa bungeni pamoja na ripoti za ukaguzi wa Utambuzi zilizowasilishwa kwenye Bodi za Wakurugenzi za Taasisi zilizokaguliwa, kuhusu Ukaguzi wa Utendaji wa Wizara ya Ujenzi na TANROADS katka kusimamia muda, gharama na ubora wa kazi za ujenzi wa barabara matokeo ya ukaguzi yameonesha Wizara ya Miundombinu pamoja na Wakala wa Barabara zinaonekana kutoridhisha kiufanisi katika kudhibiti muda wa utekelezaji, gharama na ubora wa kazi katika miradi ya ujenzi wa barabara.

Ukaguzi mwingine wa ufanisi kuhusu Ufuatiliaji, tahmini na mgao wa bajeti katika shughuli za utoaji huduma ya afya kwa mama wajawazito ukaguzi umebaini Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii haijajihusisha kikamilifu kufuatilia shughuli za huduma ya afya kwa wajawazito. Ufuatiliaji na tahmini katika utoaji wa huduma ya afya kwa wajawazito haufanyiki kiufanisi. Mgao wa fedha katika ngazi mbalimbali za utoaji huduma hii haulengi kupunguza tatizo hili.

Ripoti hii ya Ufuatiliaji, tahmini na mgao wa bajeti katika shughuli za utoaji huduma ya afya kwa mama wajawazito imeshinda kwenye ushindani wa kimataifa na kutunukiwa “The Swedish National Audit Office (SNAO) Best Perfomance Report of the Year 2010”.

Katika ripoti za ukaguzi wa Utambuzi zilizochunguza Mfumo wa ndani wa udhibiti katika kuzuia udanganyifu na aina nyingine za makosa katika idara ya Ushuru forodha matokeo yameonesha hakuna taratibu zilizowekwa kwa ajili ya kushughulikia taarifa zinazohusu utendaji usioridhisha zilizopatikana kutoka kwenye sanduku la maoni na kupitia simu isiyo na gharama kwa mpigaji.
Ripoti kamili zinapatika kwenye tovuti hii.