Kuteuliwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Kabla ya uhuru wa Tanganyika Ofisi ilifahamika kama Idara ya Ukaguzi ndani ya Tanganyika na Kiongozi wa Ofisi hiyo alitambulika kama Mkurugenzi wa Ukaguzi. Mkurugenzi huyo aliteuliwa na Katibu wa Jimbo au Gavana Mkuu kwa maelekezo ya Katibu wa Jimbo kwa niaba ya Mfalme au Malkia wa Uingereza.
Mapema kabla ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 baada ya sheria ya Exchequer and Audit Ordinance ya mwaka 1961 jina la taasisi lilibadilishwa kutoka Idara ya Ukaguzi na kuwa Idara ya Malipo na Ukaguzi (Exchequer and Audit Department), pia jina la Mkuu wa Taasisi lilibadilika kutoka Mkurugenzi wa Ukaguzi na kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Wakati wa uhuru mamlaka ya uteuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yalikuwa kwa Gavana kwa kuzingatia ushauri wa Waziri Mkuu wa Tanganyika wakati huo. Mwaka 1962 iliundwa Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ambayo pia ilitambua uwepo wa Ofisi. Katiba hiyo ilibadilisha Mamlaka ya uteuzi kutoka kwa Gavana na kuwa mwanzo wa kuwepo kwa Mamlaka ya kikatiba ya Rais kumteua mkuu wa taasisi. Hata katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua mamlaka ya Rais kumteua mkuu wa taasisi hii.