Dira
Kuwa Taasisi yenye Kuaminika na ya Kisasa katika Ukaguzi wa Umma inayotoa Huduma za Ukaguzi za Viwango vya Juu zinazoimarisha Imani kwa Umma.

Dhima
Kutoa huduma za Ukaguzi zenye Kiwango cha Juu kwa njia za Kisasa zenye Kuimarisha Uwajibikaji na Uwazi katika Usimamizi wa Rasilimali za Umma.

MOTTO
“Modernizing External Audit for Stronger Public Confidence”.

Misingi ya Maadili

  • Kufanya kazi kwa uhuru na bila upendeleo.
  • Kufanya kazi kwa utaalam.
  • Kufanya kazi kwa uadilifu.
  • Kufanya kazi kwa ubunifu na uvumbuzi.
  • Kufanya kazi kwa kuzingatia matokeo.
  • Kufanya kazi kwa ushirikiano.

Mamlaka

Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ni taasisi Kuu ya ukaguzi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Mamlaka yake yameainishwa wazi katika Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kutanabaishwa katika Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 na 12 ya mwaka 2008.

Mamlaka, Majukumu na Wajibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali  yameainishwa kupitia Katiba tatu zilizopita za Tanganyika na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya uhuru. Katiba zinazorejewa ni Katiba ya Tanganyika ya Mwaka 1962, Katiba ya Mpito ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1965 na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Katiba hizi tatu zimeelezea wazi Mamlaka, Majukumu na Wajibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwa na na jukumu la kudhibiti matumizi ya fedha zinazotoka katika Mfuko Mkuu wa Serikali na kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha hizo. Katiba hizi zimefafanua pia juu ya mamlaka ya CAG kama vile kuwa na uhuru wa kupatiwa vitabu vya Hesabu  na taarifa nyingine zinazohitajika kwa ajili ya ukaguzi. Aidha, Katiba hizi zimeainisha uhuru wa CAG katika kutekeleza majukumu yake kuwa hatalazimika kufuata maelekezo kutoka Idara yoyote ya Serikali au mtu yeyote   wakati wa kufanya kazi yake ya ukaguzi.  Vifungu vinavyohusu mamlaka ya CAG kikatiba vimefafanuliwa ndani ya hizi Katiba tatu tofauti na kutanabaishwa katika Sheria tatu ikijumuisha:

Sheria ya kwanza ya Bunge iliyofahamika kama Exchequer and Audit Ordinance ya mwaka 1961, ambayo ilianza kutumika rasmi tarehe 1 Julai, 1961. Sheria hii ilifutwa na kubadilishwa kuwa Sheria ya Fedha ya Umma, No 6 ya mwaka 2001. Mnamo 2008 ilionekana haja ya kuwa na Sheria huru itakayoongoza na kusimamia masuala ya ukaguzi nchini. Hii ilikuwa kwa mujibu wa Tamko la Lima la mwaka 1977  la Taasisi za Juu za Ukaguzi wa hesabu Duniani ( Lima Declaration for Supreme Audit Institutions)  lililoonesha hitaji la kuwepo kwa sheria  itakayosimamia masuala ya ukaguzi na kuhakikisha masuala ya uwazi na uwajibikaji yanazingatiwa.  Kwa muktadha huo Sheria ya Ukaguzi wa Umma namba 11 ya mwaka 2008 ilitungwa na kuanza kutumika. Sheria zote hizi zinaainisha Mamlaka, majukumu na Wajibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Sheria zinampa malaka CAG  ya kuchunguza na kufanya ukaguzi wa taarifa za fedha za Maafisa Masuuli wote kuhusiana na mapato na matumizi kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika kutekeleza jukumu hili, CAG ana mamlaka ya kumwita Afisa Masuuli yeyote kwa ajili ya kutoa maelezo au taarifa. Pia CAG ana mamlaka ya kuidhinisha mtu yeyote kutekeleza jukumu la kitaaluma la mhasibu au Ukaguzi au fani nyingine yoyote katika kufanya uchunguzi au ukaguzi na ana mamlaka ya kutoruhusu malipo yoyote yaliyofanywa kinyume cha sheria.

Tofauti kuu kati ya Sheria ya mwaka 1961 ‘’Exchequer na Audit Ordinance’’ na Sheria ya Fedha ya Umma ya mwaka 2001 ni kwamba ile ya zamani ilizingatia ukaguzi wa taarifa za fedha peke yake wakati ya mwaka 2001 imeongeza wigo wa ukaguzi kwa kujumuisha ukaguzi wa thamani ya fedha. Aidha, Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 imeongeza kutanua wigo kwa kuongeza ukaguzi wa Kiuchunguzi, ukaguzi wa mazingira na kaguzi nyingine.