Historia ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Kabla na Baada ya Uhuru
Historia ya Ofisi hii inahusiana kwa karibu na historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya Mkutano wa Berlin wa mwaka 1885, sehemu ya ardhi ambayo kwa sasa ni Tanzania Bara iligawiwa kwa Wajerumani. Mwaka 1897, eneo hili liliitwa Himaya ya Ujerumani ya Afrika Mashariki na lilikuwa koloni la Ujerumani mpaka mwaka 1919. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, kupitia Mkataba wa Versailles, Waingereza walipewa haki ya kulitawala eneo hili, ambalo wakati huo lilianza kuitwa Tanganyika. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia mwaka 1946, Tanganyika iliwekwa chini ya Mamlaka ya Umoja wa Mataifa chini ya uangalizi wa Uingereza.
Desemba 1961, Tanganyika ilipata uhuru wake kutoka kwa Waingereza na kuendelea kuwa sehemu ya Jumuiya ya Madola. Mwaka 1962, Tanganyika ikawa Jamhuri. Tanganyika iliungana na Zanzibar tarehe 26 Aprili 1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Huduma za Ukaguzi Wakati wa Ukoloni
Kabla ya mwaka 1954, chombo kilichokuwa kinasimamia masuala ya ukaguzi katika himaya za Uingereza kiliitwa Ofisi ya Huduma za Ukaguzi katika Makoloni. Baadaye ilibadilishwa jina na kuitwa Ofisi ya Huduma za Ukaguzi Ughaibuni na ilijumuisha watu wote walioteuliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza kufanya kazi za ukaguzi kuanzia mwaka 1954. Kiongozi wa Ofisi hii aliitwa Mkurugenzi wa Huduma za Ukaguzi. Makao Makuu ya Ofisi yalikuwa katika Jengo la Queen Anne’s Chambers, Dean Farrar Street, Jijini London, Uingereza.
Mkurugenzi wa Ukaguzi aliwajibika kwa Waziri wa Mambo ya Nje na alipewa mamlaka ya kusimamia ukaguzi wa masuala ya umma katika makoloni yote ya Uingereza. Sehemu zote zilizokuwa makoloni ya Uingereza ziliitwa sehemu za ukaguzi katika mfumo wa kikoloni wa ukaguzi. Maafisa wa ukaguzi waliteuliwa, kupandishwa vyeo, na kupelekwa katika sehemu nyingine za kazi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza baada ya kupokea mapendekezo ya Mkurugenzi wa Ukaguzi.
Masuala ya ukaguzi yaliongozwa na maelekezo ya Waziri wa Mambo ya Nje yaliyotolewa kwa kuzingatia Maelekezo ya Jumla na Kanuni za Ukaguzi Ughaibuni. Wakati huo, watumishi wa ofisi hii waligawanywa katika makundi matatu: Maafisa wenye ajira za kudumu na pensheni kutoka Ulaya, wasaidizi wenye ajira za kudumu na pensheni wa kiasia, na wasaidizi wa Kiafrika.
Mabadiliko katika Ofisi
Kabla ya ukoloni na muda mfupi baada ya uhuru wa Tanganyika, majukumu yanayotekelezwa na Ofisi ya Taifa kwa sasa yalikuwa chini ya Kitengo cha Ukaguzi ambacho kilikuwa sehemu ya Ofisi za Huduma za Ukaguzi Ughaibuni chini ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza. Kiongozi wa Ofisi hii alikuwa Mkurugenzi wa Ukaguzi chini ya Sheria ya Ukaguzi (Sura ya 86) iliyoongoza masuala ya ukaguzi tangu mwaka 1957.
Wakati huo, Ofisi ilikuwa mtaa wa Kivukoni, Dar es Salaam, na ilikuwa na jukumu la kukagua masuala yote ya serikali ya kikoloni ambayo yalikuwa chini ya serikali kuu. Tawi la kwanza la Ofisi lilifunguliwa mkoani Arusha ili kusimamia mali zilizoachwa na Wajerumani baada ya kuondolewa Tanganyika. Baadaye, matawi mengine yalifunguliwa katika mikoa ya Mwanza na Tanga, na makao makuu yaliendelea kubaki Kivukoni, Dar es Salaam.
Tarehe 1 Julai 1961, miezi minne na siku nane kabla ya Uhuru wa Tanganyika, Sheria ya Maduhuri na Ukaguzi, 1961 ilitungwa na wakoloni. Sheria hii ilibadili jina la Ofisi kuwa Idara ya Ukaguzi inayoongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Mamlaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu yaliendelea kutambulika baada ya uhuru kupitia Katiba ya Tanganyika (Ibara ya 73) na majukumu makuu yakiwa ni udhibiti na ukaguzi. Mwaka 1962, Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ilitungwa na kuanzisha mfumo wa urais wenye mamlaka. Mamlaka ya uteuzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu yalihamishiwa kwa Rais. Utaratibu huo uliendelea katika Katiba ya Mpito ya mwaka 1965 na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo imeendelea kutambua mamlaka, majukumu, na uhuru wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Kufuatia mabadiliko kwenye uchumi wa nchi na uhitaji wa maboresho ya udhibiti na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma, Sheria ya Fedha za Umma ilitungwa na kufuta Sheria ya Maduhuri na Ukaguzi ya mwaka 1961. Sheria hii ilifafanua masuala ya ukaguzi na kulitambua jina la ofisi kuwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
Mwaka 2008, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwa na sheria mahususi inayosimamia masuala ya ukaguzi na inayohakikisha uwajibikaji katika matumizi ya raslimali za umma, Serikali ilipendekeza sheria ya Ukaguzi wa Umma inayozingatia vigezo vya kimataifa vya utendaji wa taasisi za ukaguzi na uhuru wake. Bunge lilitunga Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008. Hatua hii ilifuatiwa na kutangazwa kwa kanuni za ukaguzi mwaka 2009.
Sheria zinazosimamia masuala ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Tanzania zinaendana na matakwa ya matamko ya kimataifa kuhusu utendaji na uwajibikaji wa ofisi hizi. Sheria ya Ukaguzi ya sasa imetamka wazi juu ya uteuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, muda wake wa utumishi na jinsi unavyolindwa, aina za kaguzi anazoweza kufanya, uhuru wake katika utendaji na masuala ya fedha. Pia imeeleza juu ya uwajibikaji katika ofisi hii, ikiwemo utaratibu wa kukaguliwa kwa ofisi hii na jinsi mkaguzi wake anavyopatikana.