Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Ludovick S. L. Utouh  amewataka wafanyakazi wake kudumisha mshikamano ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Akimkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Joel Bendera, ili kufungua Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) CAG alisema kila mfanyakazi anapaswa kutambua umuhimu wa mwenzake katika kufanikisha na kufika dira ya Ofisi. Ofisi haitakuwa tayari kufanya kazi na watumishi wazembe na wavivu wasiotayari kushirikiana na kufanyakazi kwa bidii ikiwa ni pamoja na kukamilisha kazi kwa wakati.

Akiendelea kufafanua CAG ulisema kuwa kutokana na NAOT kuchaguliwa kukagua Umoja wa Mataifa (UN) kuanzia Julai mosi mwaka huu asingependa wakaguzi kutoka ofisi yake kuonesha uzembe kwenye utekelezaji wa jukumu hilo lenye heshima kubwa katika nchi yetu, ulimwenguni na katika Ofisi yake.  Ukaguzi wa Umoja wa Mataifa (UN) usipotekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu unaweza kushusha imani kubwa waliyonayo Umoja wa Mataifa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi katika usimamizi wa rasilimali za umma.

Novemba mwaka jana CAG wa Tanzania aliteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Ukaguzi wa Umoja wa Mataifa (UNBOA) ambapo Tanzania kushirikiana na China na Uingereza inaunda Bodi hiyo.

NAOT imeshateua wakaguzi 60 kutoka katika Ofisi yake kwenda kufanya ukaguzi wa Umoja wa Mataifa tangu Julai mosi mwaka huu. Aidha, CAG aliwajulisha wajumbe wabaraza kuwa  nafasi hii ya kukagua UN itaoa fursa kubwa kwa watumishi wa NAOT kujenga uwezo na kuaminiwa kimataifa. Vilevile, aliwajulisha wajumbe kuwa uteuzi wa wakaguzi wa UN utakuwa wakubadilika ili kutoa fursa kwa wakaguzi wengi kupata uzoefu wa kimataifa.

Akifungua mkutano wa baraza la wafanyakazi la ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Joel Bendera ametoa changamoto kwa wakaguzi nchini kutimiza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na ujasiri bila kuogoapana ili kulinda rasilimali za nchi. Mhe. Bendera aliisifu Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa kazi nzuri inayozaa matunda yanayoonekana siku hadi siku. Alimshukuru CAG kwa Ukaguzi Maalum wa wilaya ya Kishapu uliobainisha kasoro nyingi na kuahidi kufanyia kazi yale yote yaliyoripotiwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali lilifanyika tarehe 11 Septemba 2012 katika hoteli ya Morogoro iliyopo mkoani Morogoro.