Mwenyekiti wa kamati ya Usimamizi wa Mahesabu za Canada (CCAF) ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Columbia, Bruce Ralston, amesema Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Kamati za Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), zinatakiwa kupewa muda mwingi wa kufanya kazi zake, kwani zina wajumbe wapya ambao lazima wapate changamoto na ndiyo sababu wameshirikiana na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali  kuendesha warsha tatu hapa nchini ili kuwasaidia viongozi hao kufanya kazi zao kwa umakini zaidi.

Akizungumza katika mafunzo hayo ya siku tatu, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe, alisema lazima vyama na wale wanaopokea fedha za umma, kuheshimu maamuzi ya kamati hizo mbili ya kuwakagua.

“Wale wasiotaka kuguswa na kamati hizi, basi wanatakiwa wasipokee fedha za umma… tumeona jinsi baadhi ya vyama vinavyokuja juu pale vinapotakiwa kutoa taratibu za hesabu zao,” alisema Filikunjombe.

Hata hivyo, Filikunjombe alisema kutokana na kamati hizo mbili kulibeba Bunge, Spika na Naibu wake wanatakiwa kutotumia maamuzi yao ya kuzivunja kamati hizo mara kwa mara ili kuitakia mema nchi.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Ludovick Utouh (CAG) alisema ofisi yake imekuwa ikifanya mahusiano mazuri na CCAF ya Canada kwa ajili kuzijengea uwezo kamati hizo mbili nchini.

“Tunatoa mafunzo kwa kamati hizi ili wawe na mbinu za kuhoji matumizi ya fedha za wananchi na kuwasilisha taarifa husika mahala husika,” alisema Utouh.

Aidha CAG Ludovick Utouh, aliongeza  kuwa ni muhimu Spika Anna Makinda akaona umuhimu wa kuleta kamati nyingine ili kuwezesha shughuli zilizokuwa zikifanywa na kamati ya POAC zikaweza kuendelezwa.

“Tunafahamu umuhimu wa kamati hiyo, leo tunaona umuhimu wa kazi zilizokuwa zikifanywa na kamati iliyovunjwa, hivyo Bunge linapaswa kuzingatia uamuzi unaofanywa,” alisema. Utouh aliongeza kuwa ni vyema Bunge likaona umuhimu wa kamati hizo ikiwa ni pamoja na kuziwezesha ili zifanye kazi zao kwa umakini.

Naye Mwenyekiti wa LAAC, Rajab Mbarouk Mohamed, alisema kuwa kamati hiyo inasikitishwa na kitendo kinachofanywa na ofisi ya Bunge kwa miaka miwili kushindwa kuwapa fedha ili kuweza kukagua miradi ya maendeleo.

Alisema kuwa hivi sasa kamati zimechoka kuwa washauri tu badala yake zimetaka kupewa meno ili ziweze kutembea na askari polisi pindi zinapokwenda kufanya ukaguzi mbalimbali.

“Ili nidhamu irudi katika halmashauri zetu tuna haja ya kupewa meno na kukabidhiwa polisi ili tunapokamata watendaji wabadhirifu tuweze kuwakabidhi kwa vyombo vya dola na wakawekwa ndani ili waogope,” alisema.

Awali mgeni rasmi Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliyewakilishwa na Naibu Spika, Job Ndugai, alimpongeza CAG Ludovick Utouh, kwa kubadilisha mahesabu ya umma na kuwa ya kimataifa.

“Ofisi inampongeza Utouh kwa kubadili mahesabu ya umma na kuonekana ya kimataifa zaidi…pia lazima maoni yaliyopendekezwa na wenyeviti wa kamati hizi yawasilishwe bungeni kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho,” alisema Ndugai.

Alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa ajili ya kuziboreshea kamati hizo katika ukaguzi wa fedha za umma.

Akijibu hoja hizo, Ndugai alikiri kuwa huko nyuma sheria za Bunge zilikuwa haziruhusu vyombo vya habari kuingia wakati idara mbalimbali zinahojiwa kuhusu matumizi.

Ndugai alisema kuwa kuanzia sasa wanajaribu kuangalia namna ya kuweka uwazi katika suala hilo ili kuviruhusu vyombo vya habari kupata taarifa za matumizi ya fedha za umma.