Naibu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CPA. Salhina Mkumba, kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CPA. Charles E. Kichere, amefungua rasmi warsha inayohusu tathmini ya mifumo ya TEHAMA katika ukaguzi wa fedha. Ufunguzi huo umefanyika leo, Agosti 25, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya White Sands jijini Dar es Salaam. Aidha, tukio hili limeandaliwa na African Organisation for English-Speaking Supreme Audit Institutions (AFROSAI-E) kwa ushirikiano na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Tanzania (NAOT) kama mwenyeji.
Warsha hii inalenga kuongeza uelewa na ujuzi wa wakaguzi wa kutathmini athari za matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika uandaaji taarifa za fedha. Pia, inatoa fursa kwa wakaguzi kujadili mbinu bora na kubadilishana uzoefu katika kuhakikisha uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma.
Mafunzo haya yanayofanyika kuanzia Agosti 25 – 29, 2025, yamekutanisha wakaguzi kutoka nchi wanachama wa AFROSAI-E zikiwemo Tanzania, Namibia, Eswatini, Ethiopia, Lesotho, Sierra Leone, Liberia na Gambia. Kupitia warsha hii, uwezo wa taasisi za ukaguzi barani Afrika unatarajiwa kuimarika zaidi ili kukabiliana na changamoto za matumizi ya mifumo ya TEHAMA na kuendeleza mshikamano wa kikanda katika kusimamia na kulinda rasilimali za umma.