Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Charles Kichere ametoa maelekezo kwa viongozi na watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuzingatia Uwazi na Uwajibikaji ili kuboresha maadili katika utumishi wa Umma. Bw. Kichere alitoa wito huo wakati akiongea na wafanyakazi katika Baraza la Wafanyakazi,lililofanyika jijini Dodoma.

CAG Kichere alisema kuwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imepewa  Mamlaka  na majukumu  makubwa  ya kikatiba  na kisheria  ambayo kwa ujumla wake yamelenga kutoa mchango  katika kuimarisha  uwajibikaji  na kuhakikisha  kuna matumizi thabiti ya rasilimali za Umma kwa niaba ya wananchi wa Tanzania.

Alisisitiza kuwa watumishi wa Ofisi hiyo wana wajibu wa kufuata kwa vitendo kaulimbiu ya KATAA RUSHWA, ZINGATIA UADILIFU NA MAADILI KATIKA UTUMISHI WA UMMA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU’ ili kusadifu maelekezo hayo.

“Kauli mbiu ya siku ya Wafanyakazi inawataka watumishi wawe na maadili katika utumishi wa Umma, hivyo watumishi wote wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wanawajibu kuenenda nayo,” alisema.

Alitoa angalizo  kwa watumishi wote watakaoenda kinyume na maelekezo hayo kuwa watachukuliwa hatua za kinidhamu.

“Sina uvumilivu katika  masuala ya kutozingatia maadili kwa Ofisi ninayoisimamia, ikitokea  kuna tuhuma  juu mtumishi yoyote kakiuka  maadili na ikathibitika basi  taratibu za kisheria  zitachukuliwa mara moja”  

CAG Kichere alitumia muda huo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuipa ushirikiano Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ikiwemo kuiongezea Bajeti kwa mwaka 2020/2021 pamoja na kupatiwa wakaguzi  30 thelathini wapya wakiwemo wakaguzi wa Tehama 12.

Awali CAG alimdokeza Mgeni Rasmi wa Baraza , Katibu Mkuu Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumushi wa Umma, Dkt Laureni Ndumbaro  kwa kusema Ofisi  ina changamoto ya watumishi Pamoja na Serikali kutupatia Watumishi 30 bado tuna uhaba wa Watumishi katika Ofisi yetu.

Kwa upande wake, Mgeni Rasmi wa Baraza hilo, Dkt Ndumbaro  alisema atashughulikia tatizo la uhaba wa Wafanyakazi kulingana na bajeti itakavyokuwa ikiruhusu.