Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ikiwa kama ofisi zingine za umma inatarajia kushiriki katika maonesho ya wiki ya utumishi wa umma yatakayofanyika kuanzia tarehe 16/6/2014 hadi tarehe 23/6/2014 katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es salaam.

Katika maonesho hayo ofisi inatarajia kuonesha namna  inavyofanya kazi zake za ukaguzi  kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ripoti mbalimbali  za miaka ya nyuma na ya sasa,  zana za ukaguzi na miongozo mbalimbali  ya ukaguzi,  kanuni za ukaguzi, vigezo mbalimbali  vya ukaguzi, katiba inayotumika kukagua, mkataba wa huduma kwa mteja na mpango mkakati wa Ofisi.

Pamoja na hayo ofisi itagawa ripoti za mwaka wa fedha unaoishia Juni 2013 na vipeperushi mbalimbali vinavyoitangaza Ofisi.

Aidha ukiwa mdau wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi unakaribishwa kushiriki katika maonesho hayo ili kuona na kujua Ofisi hii inafanya nini katika kudhibiti  na kusimamia rasilimali za umma.

Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo: “Mkataba wa Msingi na Kanuni za Utumishi wa Umma Barani Afrika ni Chachu ya Kuimarisha Utawala Bora na Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi”