Ofisi ya Taifa ya ukaguzi wa Hesabu za Serikali, (NAOT) imeanza mafunzo ya wiki moja kwa wakaguzi wake wapatao 120 yanayofanyika katika hoteli ya Giraffe Jijijni Dar es Salaam yenye lengo la kuwajengea uwezo ili kuwasaidia wakaguzi hao katika kazi zao za kila siku za ukaguzi.
“Ofisi yetu ni miongoni mwa Taasisi zinazoongoza katika kuwajengea uwezo wafanyakazi wake kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi. Wadau na Serikali yetu kwa ujumla wamekuwa makini katika kuhakikisha kwamba kwa pamoja tunapata mafunzo na kutimiza majukumu ya kikatiba”
Hayo yamesemwa na Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Bwana Francis Mwakapalila, wakati akifungua mafunzo ya wiki moja ambayo yameanza leo tarehe 21, Oktoba na kutegemea kumalizika tarehe 25, Oktoba, 2013 huku akiwataka wakaguzi hao kusoma kwa makini na kuzingatia wanayofundishwa.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo , Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa NAOT Mama Salome Mollel, pia amewataka wakaguzi hao kusoma kwa bidii kwa sababu lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo na kuongeza ufanisi katika kazi zao za kila siku za ukaguzi.
Mafunzo hayo yanayotolewa na wakufunzi kutoka Ofisi ya Ukaguzi ya India, yana lengo la kuwajengea uwezo wakaguzi hao kwa upande wa ukaguzi wa mapato, ukaguzi wa IT, na Ukaguzi wa Umma jinsi gani wataifanya kazi yao kwa umakini zaidi na kupata matokeo mazuri zaidi wakati wa ukaguzi wanaoufanya kila wakati.