Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Ludovick S. L. Utouh amesema ofisi yake inafanya kazi kwa uangalifu mkubwa ili kubaini mianya mbalimbali ya ubadhirifu wa fedha za umma. Akifafanua katika semina ya waandishi wa vyombo vya habari na taasisi zisizo za kiserikali alisema katika miaka sita iliyopita, Ofisi yake imewezesha baadhi ya wizara, mikoa na taasisi za umma kubadilika na kufanya kazi kwa uangalifu mkubwa.

“Ofisi yangu ipo kikatiba kwa hiyo tunafanya kazi kwa uangalifu mkubwa, hakuna wa kutuzuia kufanya ukaguzi mahali popote na katika hili, ofisi zote za serikali zinakaguliwa kwa maana hiyo hakuna haja ya watanzania kuhofia utendaji wetu. Ukilinganisha na miaka sita iliyopita kwa sasa kuna maboresho makubwa ya matumizi ya fedha za serikali katika wizara, mikoa na mashirika ya umma.” alisema Bw. Utouh.

Akieleza tatizo la rushwa nchini alisema rushwa bado ni tatizo kubwa hapa nchini na hivyo kuna haja ya kila taasisi kuongeza umakini katika kushughulikia tatizo hilo badala ya kuachiwa watu ama taasisi chache tu.

Akiongea na washiriki wa semina hiyo mmoja wa wawezeshaji katika semina hiyo Bw. Ayub Rioba ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam,  alisema hali ya umasikini inayoendelea nchini ni matokeo ya kukithiri kwa rushwa katika sekta mbalimbali za serikali. “Tafiti zinaonyesha umasikini unaendelea ambako watu milioni 270 mpaka 340 wataendelea kuwa masikini na asilimia 40 kati yao wanaishi kwa mlo mmoja kwa siku” alisema Rioba.

CAG aliona kuna umuhimu wa waandishi wa habari kupewa mafunzo maalum kuhusiana na ripoti zake ili kuwajengea uwezo wa kutosha kutoa taarifa hizo kwa ufasaha zaidi.  Semina hiyo iliyofunguliwa na Balozi wa Uingereza nchini ilifanyika Ijumaa ya tarehe 14 Septemba, 2012  katika hoteli ya Belmonte iliyopo katikati ya jiji la Dar es salaam na kudhaminiwa na DFID pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.