Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Ludovick Utouh ameanza kukagua hesabu za mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni 2010. Hesabu hizi ziliwasilishwa na wizara, idara, wakala na taasisi mbalimbali za serikali katika ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali mwishoni mwa mwezi Septemba, mwaka huu.

Aidha, ripoti za ukaguzi wa hesabu hizo kulingana na ibara ya 143 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (iliyorekebishwa 2005) na kifungu cha 34(1)(C) cha sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008 zitawasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwishoni mwa mwezi Machi ili kupelekwa bungeni kwa uchambuzi mwezi Aprili.

Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAO) ilianzishwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (Iliyorekebishwa 2005) ibara ya 143 ambapo madaraka na wajibu wake umeelezwa na kufafanuliwa zaidi katika kifungu cha 10 (1) cha sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008. Kwa mujibu wa ibara ya 143(2) (C) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anatakiwa angalau mara moja kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, hesabu zinazosimamiwa na watumishi wote wa Serikali ya Jamhuri wa Muungano na hesabu zinazosimamiwa na Katibu wa Bunge.

Ilikukidhi matarajio ya Bunge na yale ya Umma kwa mapana zaidi, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali inaendelea kufanya ukaguzi kwa kulenga na kuyapa kipaumbele maeneo muhimu ili kuchangia kuimarisha utoaji wa taarifa za usimamizi wa fedha na masuala ya utawala bora.