WAFANYAKAZI WASTAAFU WAAGWA HUKU WAFANYAKAZI BORA NA HODARI WAKIKABIDHIWA ZAWADI ZAO

Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) imefanya hafla ya kuwaaga Watumishi waliostaafu pamoja na kukabidhi zawadi kwa Wafanyakazi bora na hodari kwa mwaka 2022. Hafla hiyo imefanyika hivi karibuni kwenye Ofisi za Makao Makuu ya NAOT zilizopo jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga Wastaafu na kuwapongeza Wafanyakazi bora na hodari, Mgeni Rasmi, Naibu Katibu Mkuu TUGHE Taifa, Bw. Rugemalira Rutatina amewapongeza Watumishi waliostaafu na Watumishi bora na hodari wa NAOT kwa mwaka 2022, ambapo amewatakia Wastaafu maisha mema na kuwataka Watumishi bora na hodari kuendelea kuchapa kazi na kwamba zawadi walizopata ziwe motisha kwao ya kuendelea na kuchapa kazi kwa tija na ufanisi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Bw. Michael Allonga amemshukuru Naibu Katibu Mkuu TUGHE Taifa kwa kuendelea kuthamini na kutoa ushirikiano kwa NAOT katika kwa ajili ya kuwezesha ufanisi katika kazi na kuwezesha maslahi bora ya watumishi.

“Wafanyakazi bora na hodari ni miongoni mwa Wanachama 292 wa TUGHE, mchujo ulikuwa mkali hasa kuwapata washindi na hasa ukizingatia kwamba NAOT ina watumishi wengi, bahati nzuri vigezo mlivyotupatia TUGHE ili vituongoze namna ya kuwapata hawa walio bora na hodari hakika vilitusaidia kuifanya kazi hii kuwa nyepesi,” amefafanua Allonga.

Pamoja na kutoa zawadi kwa Watumishi bora na hodari, Menejimenti pia iliwaaga Watumishi ambao wamestaafu rasmi utumishi ndani ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa heshima kubwa. Watumishi ambao wamestaafu ni pamoja na Dereva Mwandamizi, Bw. Reinfrey Vitus Matepo, Mkaguzi Msaidizi wa Hesabu Daraja La II, Bw. Matatizo Togoka Mwampashe na Msaidizi wa Mtendaji Mkuu Daraja La I, Bi. Agness Mutakyawa.

Watumishi wote waliostaafu wametajwa kuwa ni mfano wa kuigwa katika utendaji kazi wa Utumishi wa Umma kwa kutekeleza majukumu yao kipindi chote cha utumishi wao kwa kuchapa kazi, kuwa na nidhamu na kuheshimu kazi kwa maslahi mapana ya Taifa na Ofisi kwa ujumla jambo ambalo limetajwa kuwawezesha kustaafu utumishi wa umma kwa heshima kubwa.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (GCU)

Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Tanzania (NAOT)

23 Juni, 2022.