Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAO) leo tarehe 28 Mei imefanya kikao kazi cha siku moja ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kuandaa mapendekezo ya utungwaji wa Kanuni za Utangazaji Mali na Madeni kwa watumishi wa Ofisi yake.

Kikao kazi hiki pia kimehudhuriwa na wadau kutoka katika Taasisi tofauti ikiwemo TAKUKURU, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sekretarieti ya Maadili ya Uongozi wa Umma.

Akifungua kikao kazi hiko kilichofanyika Mkoani Singida Bwana Omary Mkomwa ambaye ni Afisa Masuuli wa Ofisi hiyo amewataka watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuhakikisha wanatimiza majukumu waliyopewa katika kukagua na kusimamia rasilimali za nchi kwa manufaa ya wote.

Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ni Taasisi kuu ya ukaguzi nchini. Ofisi hii inao wajibu wa kipekee katika kusimamia uwajibikaji na uadilifu kwa watumishi wake katika matumizi ya rasilimali za nchi.

Aidha Bwana Mkomwa ameongeza kwa kusema kuwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inao wajibu wa kipekee katika kusimamia uwajibikaji na uadilifu kwa watumishi wake katika rasilimali za nchi. Amesisitiza kwamba watumishi hao wanapaswa kuwa kioo na mfano wa kuigwa katika suala la uadilifu.

Ameeleza kuwa ili kuboresha uadilifu wa watumishi inaonekana ni vyema kutungwa kwa kanuni za watumishi kutangaza mali na madeni yao. 

Kikao kazi hiko kimefanyika kwa uwezeshaji wa Serikali ya awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mh. Dr. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mradi wa kujenga uwezo uendelevu wa kupambana na rushwa Tanzania (Building Sustainable Anti-Corruption Action Tanzania – BSAAT) uliofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la DFID Department for International Development na Umoja wa Ulaya (EU).