Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG Ludovick Utouh ameishauri Serikali kuangalia upya  vyanzo vya mapato na matumizi ya fedha za Serikali kwa kuwa ni dhahiri  hali ya fedha si nzuri kabisa.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu aliyasema hayo  wakati akifungua Mkutano wa pili wa mwaka wa kipindi cha fedha 2013-2014 wa Baraza Wafanyakazi la Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali jijini Dodoma.

Mwaka wa fedha 2013/2014 Serikali imekuwa na bajeti iliyoidhinishwa Juni 2013 tofauti na kipindi kingine ambapo bajeti ilikuwa ikiidhinishwa  mwezi Julai.

Aidha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu alisema kuna uhaba mkubwa sana katika kada ya Ukaguzi  kutokana na ongezeko la kazi za Ukaguzi wa Umoja wa Mataifa na upanuzi wa shughuli za Serikali ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Mikoa mipya minne ambayo ni Katavi, Njombe, Geita na Simiyu na Halmashauri 19, Ofisi inahitaji wakaguzi zaidi ya 500 kwa ajili ya ukaguzi wa serikali za mitaa na Tawala za Mikoa ikilinganishwa na wakaguzi 278 waliopo sasa.

Alisema Serikali imeunda maeneo mapya ya utawala kwa kuanzisha mikoa mipya.

CAG aliongeza kuwa, Ofisi yake imeshaiomba Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma iruhusu angalau ajira 100 za wakaguzi wa Daraja la pili na tayari barua hiyo imeshawasilishwa.Wkaguzi hawa wataziba mapengo katika maeneo mengi ya ukaguzi ambayo hayafikiwi na wakaguzi kutokana na uhaba huo.

Mdibiti na Mkaguzi Mkuu kwa mara nyingine ameomba ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuboresha maslahi ya Watumishi wa ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ili kuwa ari ya kazi  na wakati huohuo ameomba kuwalegezea masharti wakaguzi wa hesabu wasaidizi wapatao 38 ambao wana uzoefu mkubwa wa kazi za kikaguzi na kwa miaka mingi  wanafanya kazi zao vizuri ili waweze kupandishwa cheo na kuwa wakaguzi Daraja la pili.