Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) imeandaa mafunzo ya siku tano kuanzia tarehe 21 - 25 Februari, 2011 kwa ajili ya kamati za hesabu za bunge zinazosimamia fedha za umma.

Mafunzo haya yatafunguliwa Jumanne, Februari 22, 2011 na Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Anna makinda katika ukumbi uliopo Kiromo View Resort – Bagamoyo.

Watakaohudhuria mafunzo hayo ni zaidi ya washiriki 70 wakiwemo wenyeviti wa kamati za hesabu za bunge, wanakamati pamoja na watendaji mbalimbali wa serikali.

Mafunzo haya yatalenga katika kukuza uelewa kwenye usimamizi wa fedha za umma, mbinu mbalimbali katika kutathimini uhalisia wa matumizi ya fedha, wajibu wa bunge katika kuimarisha uwajibikaji, sheria ya fedha za umma, sheria ya ukaguzi wa umma, sheria ya manunuzi na wajibu wa bunge katika uwajibikaji na uwazi katika masuala ya fedha.