Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaendesha warsha ya siku mbili na Waandishi wa Habari  Mkoani Mwanza. Warsha hii ina lengo la kuwajengea washiriki uwezo katika kuripoti taarifa za ubadhilifu zinazotokana na ripoti za ukaguzi zinazotolewa na ofisi hiyo.

Ofisi inatarajia mafunzo haya yatasaidia kuviwezesha vyombo vya habari kufikisha kwa umma taarifa zinazohusu ripoti za kikaguzi zinazotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na zinawafikia wananchi kwa usahihi kama zinavyotakiwa.

Warsha hii inafadhiliwa na program ya Kujenga Uwezo Endelevu wa Kupambana na Rushwa Tanzania (Building Sustainable Anti- Corruption Action Tanzania (BSAAT) ambayo ofisi inashiriki katika utekelezaji wake. Taasisi nyingine zinazoshiriki ni Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sekretariati ya Maadili ya Viongozi, Ofisi ya Msajili wa Leseni na Biashara, Ofisi ya Utawala Bora na Maboresho pamoja na Mahakama.

Moja ya lengo la programu ni kuwajengea uwezo watumishi wa ndani wa ofisi na watumishi wa  sekta zingine za umma pamoja na wadau mbalimbali ikiwemo waandishi wa habari.

Pia programu hii ina lengo la kujenga mfumo thabiti wa udhibiti wa rushwa, kupitia na kuhuisha nyaraka mbalimbali na kuboresha mazingira ya utendaji kazi ili kudhibiti rushwa ikiwa pamoja na ufuatiliaji wa utekelezaji na kufuata miongozo mbalimbali  iliyoandaliwa.

Programu hii ya BSAAT inafadhiliwa na Serikali ya Uingereza/Northen Ireland kupitia Shirika lake la Maendeleo (DFID) pamoja na Umoja wa Ulaya (EU) kwa ajili ya utekelezaji.

Program hii ya miaka mitano ilianza kutekelezwa rasmi mwezi Septemba, 2018 na itaendelea mpaka mwaka 2023. Usimamizi na uratibu wa mradi huu upo chini ya Ofisi ya Rais Ikulu.

Akifungua Warsha hiyo Msaidizi wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Anna Masanja kutoka Kanda ya Ziwa alisema,’Ni imani yangu mkielewa vizuri  mtatusaidia sana katika kuwaelewesha wadau na Wananchi kwa Ujumla namna ya kusimamia rasilimali na fedha kwa ajili ya maendeleo  ya Taifa letu; pia kwa kupitia vyombo vyenu  mtatusaidia sana katika kuchambua kwa ufasaha kutumia lugha nyepesi ambayo kila mwananchi ataweza kuelewa vizuri na kufanya maamuzi sahihi ya kusimamia matumizi ya Raslimali za Taifa,  Ninyi ni wadau muhimu na tunawategemea sana”