OFISI YA TAIFA YA UKAGUZI YATOA MSAADA KWA KITUO CHA KULEA WATOTO CHA KIJIJI CHA MATUMAINI DODOMA

Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) wamekabidhi msaada kwa kituo cha watoto yatima kilichopo Kijiji cha Matumaini jijini Dodoma. Msaada huo umekabidhiwa kwa mlezi wa Kituo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo huadhimishwa mwezi Juni kila mwaka.

Akizungumza kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Naibu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali – Divisheni Serikali za Mitaa, Bw. Benjamin Mashauri amesema utoaji wa msaada huo ni sehemu ya hatua mbalimbali zilizopendekezwa katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2022.

“Kwa namna ya pekee naomba upokee salamu za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ambae anatambua kazi kubwa mnayoifanya katika kituo hiki ya kulea watoto na Ofisi yetu itaendelea kutoa misaada kwa jamii kadri itakavyowezekana,” amefafanua zaidi Mashauri. Msaada uliotolewa kwa kituo ni pamoja na mchele, sukari, maji ya kunywa, maziwa ya unga aina ya lacktojeni kwa watoto wachanga, sabuni za kufulia, sabuni za kuogea, mafuta ya kupikia, soda, juisi na zawadi nyingine za kuwapa watoto faraja.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni moja ya matukio muhimu katika kalenda ya Umoja wa Afrika (AU) ambapo nchi wanachama huadhimisha kwa kufanya maonyesho ya kazi mbalimbali na Kongamano kuhusu masuala ya Utumishi wa Umma. Moja kati ya shughuli zilizotekelezwa katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka huu ilikuwa ni pamoja na kufanya shughuli za kijamii ili kujenga mahusiano mazuri na Wananchi.

Kwa kutambua kwamba Kijiji cha Matumaini kinatoa mchango mkubwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha ustawi wa jamii hususani katika kulea na kutunza watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu. Mbali na kukabidhi msaada huo wa Ofisi, Wafanyakazi walioshiriki kwenye tukio hilo waliendesha harambee fupi na kukusanya zaidi ya Shilingi Milioni 1 na laki 4 ambazo walizikabidhi kwa Kituo ili ziweze kusaidia mahitaji ya Kituo.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (GCU)

Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Tanzania (NAOT)

24 Juni, 2022.