Historia ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Kabla na baada ya Uhuru
Historia ya Ofisi inaenda kwa ukaribu na historia ya Taifa la Tanzania. Baada ya Mkutano wa Berlin wa Mwaka 1885, sehemu ya ardhi ambayo kwa sasa ni Tanzania Bara iligawiwa kwa Wajerumani. Mwaka 1897,eneo hili lilitwa himaya ya Ujerumani ya Afrika Masharriki na lilikuwa koroni la Ujerumani mpaka mwaka 1919. Baada ya vita vya kwanza vya dunia, kupitia Mkataba wa Versaille, Waingereza walipewa haki ya kulitawala eneo hili ambalo wakati huo lilianza kuitwa Tanganyika. Baada ya vita vya pili vya dunia mwaka 1946, Tanganyika iliwekwa kama eneo lilochini ya Mamlaka ya Umoja wa Mataifa chini ya unangalizi wa Uingereza.
Desemba 1961, Tanganyika ilipata uhuru wake kutoka kwa Waingereza na kuendelea kuwa sehemu ya Jumuiya ya Madola na mwaka 1962 Tanganyika ikawa Jamhuri. Tanganyika iliungana na Zanzibari tarehe 26 Aprili 1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Huduma za Ukaguzi wakati wa Ukoloni
Kabla ya Mwaka 1954 chombo kilichokuwa kinasimamia mausuala ya Ukaguzi katika himaya za Uingereza iliitwa Ofisi ya huduma za ukaguzi katika makoloni. Baadae ilibadilishwa jina na kuitwa Ofisi ya Huduma za Ukaguzi ughaibuni na ilijumuisha watu wote walioteuliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza kufanya kazi za ukaguzi kuanzia mwaka 1954. Kiongozi wa Ofisi hii aliitwa Mkurugenzi wa Huduma za Ukaguzi. Makao makuu ya Ofisi yalikuwa Jengo la Queen Anne’s Chambers, Dean Farrar Street, Jijini London nchini Uingereza.
Mkurugenzi wa Ukaguzi aliwajibika kwa Waziri wa Mambo ya Nje na alikasimiwa mamlaka ya kusimamia ukaguzi wa masuala ya umma katika makoloni yote ya Uingereza.
Sehemu zote zilizokuwa makoloni ya Uingereza ziliiitwa sehemu za ukaguzi katika mfumo wa kikoloni wa ukaguzi. Maafisa wa ukaguzi waliteuliwa, kupandishwa vyeo na kupelekekwa katika sehemu nyingine za kazi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza baada ya kupokea mapendekezo ya Mkurugenzi wa Ukaguzi.
Masuala ya Ukaguzi yalisimamia na maelekezo ya Waziri wa Mambo ya Nje yaliyotolewa kwa kuzingatia Maelekezo ya Jumla na Kanuni za ukaguzi ughaibuni.
Wakati huu, Watumishi wa Ofisi hii waligawanywa katika makundi matatu ambayo ni Maafisa wenye ajira za kudumu na pesheni kutoka ulaya, Wasaidizi wenye ajira za kudumu na pensheni wa kiasia, na Wasaidizi wa Kiafrika.
Mabadiliko katika Ofisi
Kabla ya ukoloni na muda mfupi baada ya Uhuru wa Tanganyika, majukumu yanayotekelezwa na Ofisi ya Taifa kwa sasa yalikuwa chini ya Kitengo cha Ukaguzi ambacho kilikuwa sehemu ya Ofisi za Huduma Ukaguzi ughaibuni chini wa Waziri wa Mambo ya nje ya Uingereza.
Kiongozi wa Ofisi hii alikuwa ni Mkurugenzi wa Ukaguzi chini ya Sheria ya ukaguzi (sura ya 86) iliyoongoza masuala ya ukaguzi tangu mwaka 1957.
Wakati huu Ofisi ilikuwa mtaa wa Kivukoni Dar es Salaam na ilikuwa na jukumu lakukagua mausala yote ya serikali ya Ukoloni ambayo yalikuwa chini ya Serikali kuu.
Tawi la kwanza la Ofisi lilifunguliwa mkoani Arusha ili kusimamimia mali za zilizokuwa chini ya Wagerumani walizoziacha baada ya kuondolewa Tanganyika. Baadae Matawi mengine yalifunguliwa katika mikoa ya Mwanza na Tanga na makao makuu yaliendelea kubaki Kivukoni Dar es Salaam.
Tarehe 1 Julai 1961 miezi minne na siku nane kabla ya Uhuru wa Tanganyika, sheria ya Maduhuri na Ukaguzi, 1961 ilitungwa na wakoloni. Sheria hii ilibadili jina la Ofisi na kuwa Idara ya Ukaguzi inaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Mamlaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu yaliendelea kutambulika baada ya uhuru kupitia katiba ya Tanganyika (ibara ya 73) na majukumu makuu yakiwa ni udhibiti na ukaguzi.
Mwaka 1962, Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ilitungwa na kuanzisha mfumo wa uraisi mwenye mamlaka. Mamlaka ya uteuzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu yalikasimiwa kwa Raisi. Utaratibu huo uliendelea katika Katiba ya Mpito ya Mwaka 1965 na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,1977 imeendelea kutambua mamlaka, majukumu na uhuru wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuguzi wa Hesabu za Serikali.
Kufuatia mabadiliko kwenye uchumi wa nchi na uhitaji wa maboresho wa uthibiti na uwajibikaji katika matumizi ya raslimali za umma, Sheria ya Fedha za Umma ilitungwa na kufuta sheria ya Maduhuri na Ukaguzi ya Mwaka 1961. Sheria hii ilifafanunua kuzungumzia masuala ya ukaguzi. Sheria ilitambua jina la ofisi kuwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
Mwaka 2008, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwa na sheria mahususi ya mausala ya ukaguzi na inayosimamia uwajibikaji katika matumizi ya raslimali za umma, Serikali ilipendekeza sheria ya Ukaguzi wa umma inayozingatia vigezo vya kimataifa vya utendaji wa taasisi za ukaguzi na uhuru wake. Bunge lilitunga sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008. Hatua hii ilifuatiwa na utangazwaji wa kanuni za ukaguzi mwaka 2009.
Sheria zinazosimamia masuala ya Ofisi ya Taifa Tanzania ya Ukaguzi kwa ujumla yanaendana na matakwa ya Matamko ya kimataifa ya yayaohusu utendaji na uwajibikaji wa Ofisi hizi. Sheria ya ukaguzi kwa sasa imetamka wazi juu ya uteuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, namna muda wake wa utumishi unavyolindwa, aina za kaguzi anazoweza kufanya,uhuru wake katika utendaji na masuala ya fedha. Pia imeeleza juu ya uwajibikaji katika ofisi hii ikiwemo utaratibu wa kukaguliwa kwa ofisi hii na namna mkaguzi wake anavyopatikana.