Kifungu cha 28 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya Mwaka 2008 kinampa mamlaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya Ukaguzi wa Ufanisi au wa Thamani ya Fedha kwa lengo la kufahamu iwapo kuna uwekevu, tija na ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma katika Wizara, Idara, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na Taasisi nyinginezo.
Kulingana na Kanuni za Ukaguzi wa Ufanisi kama zinavyotajwa katika Kifungu cha 300 cha Kanuni za Kimataifa za Taasisi Kuu za Ukaguzi wa Hesabu, Ukaguzi wa Ufanisi ni tathmini huru, isiyoegemea upande wowote inayoangalia iwapo shughuli za serikali, mifumo, utendaji, programu, shughuli au mashirika yake yanafanya kazi kwa kuzingatia kanuni za uwekevu, tija na ufanisi na iwapo kuna uwezekano wa kuwa na maboresho zaidi.