Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Edward Kichere leo tarehe 26 Machi, 2020 amemkabidhi Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ripoti ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 June 2019.

Ripoti hiyo imewasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.

Miongoni mwa ripoti zilizokabidhiwa kwa Mheshimiwa Rais ni Ripoti ya Ukaguzi wa Serikali kuu, Ripoti ya Ukaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma, Ripoti ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo, Ripoti ya Ukaguzi wa Mifumo ya Tehama, Ripoti ya Ukaguzi wa Ufanisi, Ripoti ya ufuatiliaji wa Mapendekezo yaliyotolewa katika Ripoti za Ukaguzi wa Ufanisi kwa Miaka iliyopita na Ripoti 12 za Ukaguzi wa Ufanisi katika Sekta mbalimbali ambazo ni

  1. Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kaguzi za Ufanisi ya mwaka 2016,
  2. Usimamizi wa Makusanyo ya Mapato kutoka kwa Makampuni ya Simu,
  3. Usimamizi wa Upatikanaji wa Umeme na Uhakika wa Utoaji Huduma za Umeme,
  4. Ufuatiliaji na Utekelezaji wa Shughuli za Manunuzi ya Umma,
  5. Usimamizi wa Miradi ya Ujenzi wa Maghala na Vihenge vya Kutunzia Mazao,
  6. Usimamizi wa Shughuli za Kinga na Chanjo,
  7. Ubora wa Shughuli za Ujenzi na Ukarabati wa Barabara za Lami Mijini,
  8. Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa ya Mifugo,
  9. Utekelezaji wa Jitihada za Kitaifa za Kupambana na Utakatishaji wa Fedha Nchini,
  10. Upatikanaji Usioridhisha wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi yenye Ubora kwa Watanzania,
  11. Ukusanyaji Mapato toka vyanzo vya ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa,
  12. Usimamizi wa Utoaji Program za Kuwajengea Uwezo Walimu Kazini.

Kwa mujibu wa kanuni ya 88 ya Kanuni za Ukaguzi wa Umma, 2009, taarifa hii inapaswa kuwasilishwa kwa Mh. Rais kabla ya tarehe 31, Machi kila mwaka.  Mara baada ya kupokea Taarifa hizi, Mheshimiwa Rais anapaswa  kumuelekeza  mtu husika  kuziwasilisha taarifa hizo katika  kikao kijacho cha  Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya siku 7 za kikao tangu siku ya kwanza ya kikao cha Bunge kinachofuata baada ya taarifa kuwasilishwa kwa Rais.

Published on: Mar 26, 2020 @ 11:39