Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imetoa mafunzo kwa wakaguzi yanayojulikana kama Ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali. Mafunzo haya yametolewa chini ya Mradi unaofadhiliwa na AfDB ambao umeleta mafanikio makubwa kwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.

Mafanikio hayo ni pamoja na:

  1. Wananchi  kushiriki katika Ukaguzi kwa kutoa maoni yao kwa uhuru kuhusu Ripoti za  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
  2. Kuboresha kazi za kikaguzi na uandaaji wa taarifa.
  3. Kuwajengea Uwezo Wabunge na Kamati za kudumu za Hesabu za Serikali kuhusu Ripoti za CAG.
  4. Kununua vitendea kazi kama vile fenicha, Kompyuta na kufanya mazingira ya kufanyia kazi kuwa mazuri.

Mgeni Rasmi wa Mafunzo hayo ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Bw. Novert Mfalamagoha ambaye alimuwakilisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Mafunzo hayo yanaendelea Mjini Morogoro na yatachukua muda wa siku tano.

Akifungua Mafunzo hayo kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Novert Mfalamagoha aliwashukuru wafadhili wa mradi huu kwa kufadhili mafunzo haya kwa wakaguzi. Pia aliishukuru Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa kuwezesha mafunzo haya kufanyika. Akiongea kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu alisema mafunzo haya yanaendeshwa na wakufunzi waliobobea ambao wako kwa ajili ya kutoa mada zitakazotusaidia katika kazi zetu za kila siku.

Alisistiza kuwa washiriki wamejiandaa kuzingatia yote yatakayofundishwa kwa ajili ya taaluma za wahusika. Jumla ya wakaguzi 35 wanatarajia kupata mafunzo haya.

Mgeni Rasmi alihitimisha kwa kuwataka washiriki watoe ushirikiano wa kutosha kwa wakufunzi ili kuweza kufanya mafunzo yaweze kutolewa kwa urahisi zaidi.