Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inafanya mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo Wabunge wa Kamati za kudumu za Bunge. Kamati hizi ni pamoja na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) Kamati ya kuhudumu ya Serikali za Mitaa (LAAC) Kamati ya Kudumu ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) pia ofisi inatoa mafunzo kwa watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi waliotoka katika idara mbalimbali katika ofisi hiyo ambapo mafunzo hayo yanafanyika katika mikoa ya Singida, Dodoma na Dar es salaam.

Miongoni mwa Washiriki wa Mafunzo ya Wabunge ni Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya PAC Mheshimiwa Naghenjwa Kaboyoka na Makamu wake Mheshimiwa Japhet Hassunga, Mheshimiwa Grace Tendega Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Makamu Mwenyekiti wake Mheshimiwa Selemani Zedi, na Mheshimiwa Atupele Mwakibete Mwenyekiti Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) na Makamu mwenyekiti wake Mheshimiwa George Malima.

Akiongea wakati wa ufunguzi kwa niaba ya Wenyeviti wengine, Mheshimiwa Naghenjwa kaboyoka amewataka Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha wanajifunza kwa umakini mkubwa katika kipindi hiki ili kujiongezea uwezo ambao utasaidia katika suala zima la ukaguzi wa miradi ya maendeleo na kuweza kuleta tija kwa nchi. ‘Hapa lazima tuwe wazalendo kwa nchi yetu wenyewe na kwa ofisi hii ambayo imegharamia mafunzo haya pamoja na wafadhili kwa kujifunza na kwa kujitoa ili tuweze kutumia elimu hii katika utekelezaji wa majukumu tuliyopewa na wananchi wa kuhakikisha fedha za Serikali zinafanya kazi yake na si kupotea.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Naibu Mkaguzi Mkuu wa Hesabau za Serikali Bwana Benjamin Majura amewasihi watumishi wa Ofisi hiyo kuhakikisha wanafuatilia na kujifunza kwa bidii ili mafunzo hayo yaweze kuwasaidia katika kazi zao za kila siku. Pia Bwana Benja Majura amewataka watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kufuatilia kwa umakini mkubwa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia wakati wa utendaji wa kazi zao za kikaguzi ili kuweza kuondoa changamoto mbalimbali hasa katika kaguzi za mifumo katika kurahisisha utekelezaji wa kazi zao za kila siku za kikaguzi.

Katika maelekezo yake Bwana Majura alisema kuwa Ofisi imeweza kugundua kwamba kuna wakaguliwa wengi wanatumia mifumo ya TANEPS kwa upande wa manunuzi na MUSE kwa ajili ya kufanya malipo hivyo ofisi ikaona ni bora kutoa elimu ili wakaguzi kufanya kwa urahisi zaidi baada ya kupata uelewa kupitia mafunzo haya. Alieleza kuwa najua nyinyi si wataalam wa mifumo hii lakini ofisi imeamua kuwajengea uelewa wa jumla katika kurahisisha ufanyaji kazi wenu.

Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ni Taasisi yenye jukumu la kufanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya Serikali, kama yanavyoidhinishwa na Bunge na kutoa taarifa Bungeni hivyo basi ofisi inafanya kazi kwa ukaribu na kamati za kudumu za Bunge ambapo ofisi ina jukumu la kuwajengea uwezo Wabunge hao ili kuwarahisishia utekelezaji wa kazi zao za ukaguzi wa miradi ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Hati ya Majukumu ya Mwaka 2018, Ofisi imepewa majukumu ya Kukagua hesabu za Wizara, Mikoa, Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji, Ofisi za Balozi za Tanzania zilizoko nje ya nchi, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, pamoja na Miradi ya Maendeleo inayogharamiwa na wafadhili, na kutoa taarifa ya ukaguzi huo Bungeni juu ya mapato na matumizi ya fedha za Umma pamoja na kujenga, kukuza na kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji katika Wizara na Taasisi za Serikali, Mikoa na Halmashauri na pia Kuhakikisha kwamba, inajiridhisha kuwa upo uwajibikaji wa kutosha katika kusimamia na kudhibiti ipasavyo ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali kama yanayoidhinishwa na Bunge.