DESEMBA 9 mwaka huu, Tanganyika iliadhimisha miaka 50 ya uhuru wake huku kukiwa na mambo kadhaa ambayo idara kama za Serikali Kuu ziliandaa na kuonyesha.

Kumbukumbu hiyo ya uhuru ilionyesha historia ya mambo mengi ambayo Watanzania wengi waliweza kujifunza na kuona. Lakini, zipo idara chache ambazo historia yake haikuwekwa wazi hasa kwa kizazi cha sasa kufahamu.

Kwa mfano, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) ni moja ya taasisi muhimu ambazo historia yake inakwenda pamoja na historia ya uhuru wa Tanganyika ikianzia zama za ukoloni hadi Tanganyika huru ya Desemba 9,1961

Kihistoria, Tanganyika ambayo ilikuwa koloni la Mjerumani na baadaye Mwingereza ilirithi ofisi hiyo ya ukaguzi ambayo kwa sasa ni taasisi nyeti inayosimamia utawala bora katika eneo la matumizi bora ya fedha za umma.

Kwa kuzingatia umuhimu wa utawala bora katika matumizi ya fedha za umma, utawala wa Mwingereza kabla ya Oktoba 1 mwaka 1954, ulikuwa na ofisi ya ukaguzi iliyojulikana kama Ofisi ya Huduma za Ukaguzi.

Badaye ofisi hiyo ikabadilishwa jina na kuwa Ofisi ya Kusimamia Huduma za Ukaguzi ikiongozwa na Mkurugenzi wa Ukaguzi ambaye aliteuliwa na gavana kwa niaba ya malkia.

Hata hivyo, baada ya uhuru, muundo wa ofisi hiyo ulibadilika kwani badala ya kuongozwa na Mkurugenzi wa Ukaguzi ikawa chini ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambaye kwa sasa ni Ludovick Utouh.
Viongozi wakuu

Utouh anasema tangu mwaka 1961 -2011 watendaji wakuu waliowahi kuiongoza taasisi hiyo ni; R.W.A McColl (1961-1963), Gordon A. Hutchinson (1964-1969). Mzalendo wa kwanza kushika wadhifa huo  ni Mohamed Aboud (1969-1996) aliyefuatiwa na Thomas  Kiama (1996-2005), Ludovick Utouh ambaye anaendelea na wadhifa huo.

Ingawa zipo changamoto nyingi, lakini ofisi hiyo ya ukaguzi wa hesabu ya taifa chini ya Utouh imeweza kufanya mambo mengi ya msingi na makubwa katika kusimamia matumizi bora ya fedha za umma kuanzia Serikali Kuu hadi za Mitaa.

Ripoti mbalimbali za mwaka za NAOT zimekuwa zikionyesha matumizi mabaya ya fedha za umma katika serikali za mitaa na hata kufichua wizi katika balozi za Tanzania zilizoko nje na hata matumizi mabaya ya fedha za umma.

Tukio kubwa la kihistoria kwa NAOT la hivi karibuni chini ya Utouh ni ukaguzi maalumu wa wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Fedha za Kigeni (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambao tayari, umefanya baadhi ya watu kufikishwa mahakamani na wengine kuhukumiwa.

Wizi wa EPA ulibainika katika hesabu za BoT za mwaka 2005/06, baada ya ofisi ya CAG kuipa kazi Kampuni ya Kimataifa ya Ernst&Young kufanya ukaguzi huo maalumu ambao, tuhuma zake za wizi zilikuwa zikipigiwa kelele na wabunge, hasa baada ya kubainika wizi wa Sh 40 bilioni uliofanywa na Kampuni ya Kagoda Agriculture kwa kisingizio cha kufanya kazi za Idara ya Usalama wa Taifa.

Baada ya mvutano mkubwa Bungeni baada ya kusitishwa ghafla kwa uchunguzi wa Kampuni ya Deloitte &Touche ya Afrika kusini, Serikali ilimpa CAG kazi ya ukaguzi na ndipo mteule wake, Kampuni ya Ernst &Young ilipoibuka na matokeo ya wizi huo wa zaidi ya Sh 139 bilioni uliofanywa na kampuni 22 huku tisa zikiwa za kigeni na 13 za wazawa.

Changamoto

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo ya ofisi yake, Utouh anataja changamoto zaidi zinazoikabili ofisi hiyo kuwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti kama ilivyo kwa taasisi nyingine za Serikali. Anasema ufinyu huo wa bajeti ni kikwazo cha kuongeza ufanisi zaidi wa kikazi.

Anasema ofisi hiyo imekuwa na majadiliano na Serikali kwa ajili ya kuboresha mishahara ya watumishi, kupata na kujenga majengo yake kwa ajili ya ofisi na kupata vitendea kazi vya kutosha ili kuongeza tija na ufanisi.

Aidha, Utouh anasema changamoto nyingine ni nguvu kazi ambayo haiendani na mzigo mkubwa na dhima ya NAOT ambayo majukumu yake yamekuwa yakiongezeka kila mwaka, kufuatia mahitaji ya usimamizi na utawala bora katika fedha za umma.

CAG anafafanua zaidi kwamba, wakati wa uhuru mwaka 1961, ofisi hiyo ilikuwa na wakaguzi 22  akiwamo mkurugenzi wa ukaguzi, naibu mkurugenzi, wakaguzi wakuu  watatu na huku pia ikiwa na wakaguzi waandamizi wanane, 10 walikuwa wakaguzi na wakaguzi wasaidizi  na watatu walikuwa ni wakaguzi, ngazi ya mafunzo.

Anaongeza kwamba, kipindi hicho pia ofisi ilikuwa na ofisi katika matawi manne, yaani Dares Salaam, Mwanza, Arusha  na Tanga. Pamoja na kuwa na matawi hayo manne bado ilipaswa kufanya ukaguzi kwa serikali nzima, kazi ambayo ilikuwa ngumu.

Kwa mujibu wa Utouh, NAOT iliendelea kukabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi na kwamba katika ripoti ya ukaguzi ya mwaka 1978/79, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipendekeza Serikalini kuongezwa kwa watumishi wa ofisi hiyo ya ukaguzi ili kufanikisha utendajikazi wa CAG kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya ukaguzi.

Anasema hoja hiyo ya upungufu wa watumishi ilitolewa pia katika ripoti ya mwaka 2000/01 ya CAG wa wakati ule, Kiama akieleza changamoto hiyo na tena Oktoba 27 , 2009, yeye (Utouh) alifikisha hoja hiyo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Utouh anasema katika maombi hayo, ofisi yake ilimwomba Waziri Mkuu kwamba Serikali iwezeshe ajira mpya 125 kwa ajili ya NAOT kila mwaka na kwamba, tayari Serikali kwa mwaka 2011/12 imekubali kuajiri watumishi  wapya 102 badala ya 125 , hivyo changamoto hiyo bado ipo.

Uhaba wa vitendeakazi

CAG anasema katika kipindi cha miaka 50 ofisi yake pia imejikuta bado ikikabiliwa na uhaba wa vitendea kazi  licha ya kwamba shughuli zake zimekuwa zikipanuka mwaka hadi mwaka.

Anataja  upungufu huo wa vitendea kazi kwamba ni pamoja na magari, mtandao wa intaneti kuunganisha ofisi zake, kamera, vinasa sauti, vifaa vya uchapishaji na vingine vya ukaguzi.

Mtendaji huyo mkuu huyo wa NAOT anasema ofisi hiyo ina ofisi 21  za mikoa, ambazo ndani yake kuna halmashauri 134, wilaya 114 , zikiwamo 22 mijini na 92  za vijijini ambako kote ofisi hiyo inafanya kazi zake kila siku.

Kwa ukubwa huu wa eneo la kubwa la nchi yetu, NAOT haiwezi kufanya kazi kwa ufanisi kwa kutumia gari moja kwa kila mkoa, na baadhi ya magari yaliyopo yana umri wa zaidi ya miaka  minane, hivyo hayawezi kufanya kazi kwa ufanisi, anaeleza Utouh.

Anasema NAOT pia inategemea mtandao wa intaneti kufanya kazi zake, lakini bado haijaungishwa katika vituo vyake vya nchi nzima huku kukikosekana pia kwa kompyuta za kutosha, vinasa sauti na kamera kwa ajili ya kuchukulia ushahidi katika ukaguzi wa fedha za umma na miradi ya wahisani.

Mafanikio

Anayataja baadhi yake kuwa licha ya changamoto, bado NAOT imefanya ukaguzi wa fedha za umma katika maeneo yote ya msingi ikiwamo vyama vya siasa, sekta za kijamii, sekta ya fedha na teknolojia.

Anasema mafanikio ambayo yameanza kuonekana ni kuongezeka kwa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kufuatia mapendekezo ya NAOT yanayotokana na ukaguzi, kufanyiwa kazi na serikali kila mwaka.

Mafanikio mengine anayataja  kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Idara ya Ukaguzi wa Ndani ambayo pamoja na mambo mengine, imekuwa ikitumika kutengeneza bajeti na mfumo wa malipo ambayo mategemeo ni kwamba inaweza kuondoa tatizo sugu la matumizi mabaya ya fedha za umma ikiwemo malipo ya watumishi hewa.

Mengine ni pamoja na kuwasilishwa kwa wakati kwa ripoti za ukaguzi kutoka NAOT, hivyo kuiwezesha Serikali na vyombo vingine vya maamuzi kufanya maamuzi husika kuhusu matokeo yaliyomo kwenye ripoti hizo.

Katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru,  Utouh anasema mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa nafasi ya Mkaguzi Mkuu Msaidizi, ambaye ana dhamana na Serikali za Mitaa (LGAs) na kuanzishwa kwa kamati za ukaguzi katika mamlaka hizo za mitaa ambazo huchochea utawala bora.

Anasema  katika uchumi, NAOT imeweza kufanikiwa kusaidia maendeleo ya sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kushiriki katika mchakato wa usimamizi wa fedha za bajeti kuu ya Serikali katika eneo la matumizi bora, kutoa mapendekezo kuhusu ukusanyaji mapato ya nchi kazi inayofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Anaongeza kuwa NAOT pia katika miaka 50 ya uhuru inajivunia kusimamia matumizi ya fedha za umma katika wizara mbalimbali, fedha za wahisani na njia bora za kuangalia matumizi ya fedha hizo kila mwaka.

Lakini, kwa kuongezea, NAOT pia imekuwa ikifanya ukaguzi maalumu pale inapoonekana kuna ulazima wa kufanya hivyo. Kwa mfano, kwa kushirikiana na Ernst&Young  NAOT ilifanya ukaguzi maalumu katika Benki Kuu (BoT) kuhusiana na malipo kwenye akaunti ya fedha za kigeni (EPA) ambao baadae ulibaini kughushiwa kwa malipo kwa kampuni 22, anaeleza Utouh.

Anasema hayo ni mafanikio katika sekta ya uchumi, kwani fedha hizo baadaye Serikali iliagiza zielekezwe katika sekta ya kilimo na kuongeza kwamba, taarifa zinaonyesha kuwa Benki ya Rasilimali (TIB) imepokea dola 16 milioni (Sh20 bilioni).

CAG pia anasema mafanikio hayo pia yanahusu utekelezaji wa mapendekezo yake ya kutaka Gavana wa BoT asiwe mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa Fedha wa taasisi hiyo nyeti ya nchi, kitu ambacho kimetelezwa.

Gavana wa sasa wa BoT, Profesa Benno Ndulu, muda mfupi baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2007 aliamua kujiondoa katika nafasi hiyo, huku pia akitangaza hatua mbalimbali za kuzuia mianya ya rushwa na ufisadi katika benki hiyo kuu ikiwa ni pamoja na kuchunguza ajira za watoto 16 wa vigogo na kupangua wakurugenzi wa matawi na makao makuu.

Anasema katika eneo hilo, gavana aliondolewa kwenye nafasi ya uenyekiti wa kamati hiyo hivyo pia, kuwezesha uanzishwa wa kamati hiyo uliachwa katika bodi ya wakurugenzi wa BoT.

Matarajio ya siku zijazo

Akizungumzia matarajio, Utouh anasema ni kuongeza ufanisi katika ukaguzi kwa kiwango cha kimataifa na vile vya Afrika kwa nchi zinazoongea Kiingereza na ushirikiano mwingine wa ukaguzi  katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo kwa nchi za Kusini mwa Afrika.

Anasema matarajio mengine ni NAOT kujenga chuo cha mafunzo eneo la Gezaulole, Kigamboni katika Manispaa ya Temeke na kuongeza kwamba, tayari ofisi imeingia mashuariano na mshauri mtaalamu kwa ajili ya kuchora na kuangalia shughuli za ujenzi.

SOURCE: MWANANCHI