Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC ) ikiongozwa na Mheshimiwa Naghenjwa Kaboyoka Mbunge wa Same Mashariki ikishirikiana na Ofisi ya Taifa ya ukaguzi wa Hesabu za Serikali imefanya ziara ya kutembelea miradi mbali mbali ya Serikali ikiwa ni sehemu ya Mafunzo kwa vitendo kwa wabunge wa Kamati za kudumu kwa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika ziara hiyo ya wiki mbili kamati imefanikiwa kutembelea mradi wa ujenzi wa kiwanda cha sukari cha Mkulazi kilichopo Morogoro vijijini katika maeneo ya Dakawa.

Mradi huo ambao upo chini ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Magereza unategemewa kuanza kuzalisha sukari mapema mwakani 2022 ambapo unategemewa kuzalisha tani 25 za sukari kwa siku.

Mradi huu umeanzishwa mahsusi kukabiliana na upungufu wa sukari nchini ambao unajitokeza kila mara. Jumla ya hekta elfu 28 zinategemewa kutumika kwaajili ya kuweka kiwanda hicho ambacho kitachukua miezi kadhaa kukamilika katika ujenzi wake.

Kampuni ya mkulazi iliyopo Morogoro vijijini ina jumla ya wafanyakazi 387 ambapo kati ya hao 300 ni vibarua.

Kampuni ya Sukari ya Mkulazi yenye ubia kati ya NSSF na Magereza ina lengo la kuzalisha sukari pamoja na miwa ambayo ipo tayari Katika mashamba yaliyopo katika maeneo hayo.

Katika ziara hii waheshimiwa Wabunge wameweza kujionea mashamba na miundombinu Mbalimbali iliyopo katika eneo hilo la Mkulazi ambapo ni sehemu ya mafunzo hayo kwa kamati za kudumu za Bunge PAC.

Pia katika ziara hii kamati ya Bunge ya PAC inaendelea kutembelea miradi ya kukagua majengo ya chuo kikuu cha Mzumbe, Barabara zilizopo Chini ya Tarura, Maabara Mtambuka katika chuo kikuu cha SUA, ukaguzi mradi wa jengo la utawala na karakana VETA, mradi wa Maji Moruwasa pamoja na miradi mingine iliyopo katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.